Ndugu zangu,
Zimenisikitisha sana, taarifa za maradhi yenye kumsibu ndugu yetu Joseph Haule, maarufu kama Profesa Jay.
Profesa Jay ni rafiki wa wengi. Ni rafiki kwangu pia. Mwingine atauliza;
Wapi mlikutana kwa mara ya kwanza?
Jibu: Ilikuwa ni Jumatatu moja ya mwezi Juni mwaka 2005. Ni siku hiyo nikiwa kando ya Kituo cha mabasi Ipogolo, Iringa, ndipo nilipokutana kwa mara ya kwanza na Profesa Jay.
Nilisimama nikipitia na kununua magazeti nje ya kibanda cha mwuza magazeti aitwaye Isike Maganga.
Nilikuwa njiani kuelekea Dar es Salaam nikitokea Iringa. Jua la asubuhi lilikuwa linawaka na baridi kali la mwezi Juni likipuliza. Ilikuwa haijatimu hata saa tatu asubuhi.
Nilikuwa peke yangu kwenye Landcruiser Hardtop ya kibaruani kwangu. Niliendesha mwenyewe.
Kabla sijatia moto gari, Bwana Isike mwuza magazeti alinijia na kuniambia;
"E bwana, kuna wale jamaa wawili pale wanaomba wakuchangie mafuta wako safarini kwenda Dar."
Oh! Ni Profesa Jay na Mr.Blue. Niliwatambua. Nikamwambia Bwana Isike awaambie ni sawa tu.
Profesa Jay ni mkubwa kiumri kuliko Mr.Blue. Nikamwona Profesa Jay alivyokuwa mnyenyekevu. Alimpisha Mr. Blue akae kiti cha mbele na mimi dereva , na yeye, Profesa Jay, alikaa kiti cha nyuma katikati.
Tukaianza safari baada ya kusalimiana. Nikaelewa, kuwa wawili hao hakuna aliyenifahamu. Basi, ikawa kwangu darasa la muziki, sanaa na maisha ya wasanii. Ni njia nzima. Profesa Jay na Mr. Blue walikuwa wametoka kwenye tamasha la muziki wa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Tumaini, Iringa.
Jamaa walikuwa wakiongea haswa. Walicheka na hata wakati mwingine kusikitika pamoja. Maana, walikuwa wakiongea juu ya muziki wao, wasanii wenzao na hata walivyokuwa wakidhulumiwa na mapromota wa muziki. Muda wote nilikaa kimya nikijielekeza kwenye gea na usukani.
" Dereva, utasimama mahali pa kunywa supu?"
Aliniuliza Mr. Blue. Kwa nilivyovalia, jeans ya bluu, raba mtoni na fulana, kweli kwa Mr. Blue nilionekana kama dereva tu niliyemwacha bosi, au nakwenda kumuwahi bosi.
Tulisimama Ruaha Mbuyuni. Hapo abiria wangu Profesa Jay na Mr.Blue walipata supu yao. Na hapo nikawaona vijana wauza vitunguu wakiwazonga kila walipokwenda. Hata kwa wakati huo, Profesa na Mr.Blue walikuwa ni celebrities- Watu maarufu na hususan kwa vijana.
Baada ya Ruaha Mbuyuni, tukiwa njiani kuitafuta Mikumi, na huku Profesa Jay na Mr. Blue wakiendelea kupiga soga lao, ndipo nikawatamkia;
"Mnajua, sisi wote tunafanya kazi kuifikia jamii, lakini wengine sisi tunaandika tu magazetini. Hatujulikani."
Mara, kutoka kiti cha kati nyuma anasikika Profesa Jay kwa sauti kubwa;
"Aah! Wewe ni Maggid Mjengwa! Unajua muda wote nikikuangalia najiuliza huyu jamaa nimemwona wapi! Yaani braza MwanaFa na mimi ni wasomaji wa makala zako za kwenye Rai!"
Kikafuatia kimya kizito. Mr.Blue alilaza kichwa kama anayetaka dereva nisimwone. Alifikiri juu ya yote walioongea mbele ya mwanahabari. Mr. Blue hakuwahi kusikia jina langu wala kusoma chochote nilichoandika.
Ni Profesa Jay aliyerudisha mazungumzo na hata kuanza kuniingiza kwenye mazungumzo. Nilijifunza mengi kwenye safari ile.
Profesa Jay na Mr. Blue hawakuwa hata na ruhusa kutoka kwangu ya kunichangia hela ya mafuta. Ni wao walionichangia maarifa mengi mapya.
Na ikatokea siku wakati Profesa Jay akiwa Mbunge wa Mikumi, basi la Upendo nililopanda kutokea Dar kwenda Iringa liliharibika mchana wa jua kali katikati ya pori. Ni kwenye milima na kona kali za Ihovi, nje kidogo ya Mji wa Mikumi.
Abiria tulikaa pale kwa saa kadhaa tukisubiri mafundi wamalize kutengeneza kilichoharibika. Tulitawanyika kwenye vivuli vya miti tukipoteza muda kwa mazungumzo ya hapa na pale.
Basi, kwenye kusubiri kule na kiu za maji, mara, ikatokea gari na kusimama mbele yetu.
Alikuwa ni Mheshimiwa Mbunge wa Mikumi, Profesa Jay. Akatwambia abiria, kuwa akiwa Mikumi alisikia kuna basi limeharibika porini, hivyo, amekuja na katuni za maji ya kunywa zitusaidie.
Profesa Jay akiwa na vijana watatu aliokuja nao, alishiriki mwenyewe pia, kwenye kugawa maji kwa abiria.
Ah! Profesa Jay akashangaa kuniona kuwa mimi nilikuwa mmoja wa abiria hao waliopokea kwa shukran mgao wa chupa za maji. Kwamba siku hiyo niliamua kutumia usafiri wa basi. Hutokea nikafanya hivyo pia.
Profesa Jay alituhisani kwa wema na kwa moyo wa ubinadamu, maana, tulikuwa ni abiria wapita njia tu jimboni mwake. Hatukuwa wapiga kura wake.
Niliposikia kuwa Profesa amelazwa Muhimbili na kuwa yu mwenye kuhitaji msaada wa chochote kile apate afueni, basi, kwanza limenigusa sana na kuhuzunika. Kwamba mwenzetu ni mgonjwa. Kwamba matibabu yake ni ya gharama kubwa sana.
Hivyo,hilo ni lenye kutuhitaji kujitoa, hata kwa kidogo tulichonacho. Aidha, ni imani ya wengi wetu, kuwa ayapitiayo Profesa Jay kwa sasa, nayo yatapita.
Maana, kwa mwanadamu, machungu ya maisha, ikiwamo maradhi, huja na kupita.
Nimepata kuusikia wimbo alioshiriki kuimba Profesa J.
Maggid Mjengwa.
Dar es Salaam.