KUKAMILIKA kwa mradi wa kupeleka umeme kwenye Kampuni ya uchimbaji madini ya dhahabu ya Geita Gold Mining Limited (GGML) kunatarajiwa kutaliwezesha Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kupata shilingi bilioni tano kwa mwezi zitakazotokana na mauzo ya umeme.
Mkurugenzi Mtendaji TANESCO, Maharage Chande, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mradi wa kupeleka umeme kwenye Kampuni ya Geita Gold Mining (GGML) ambao utaiwezesha TANESCO kupata shilingi bilioni tano kwa mwezi. Katikati ni Makamu wa Rais wa GGML, Simon Shayo.
Hayo yamebainika juzi Februari 21, 2022 wakati wa shughuli ya utiaji saini mkataba wa mauziano ya nishati ya umeme kati ya TANESCO na GGML.
Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika mjini Geita, Mkurugenzi Mtendaji TANESCO, Maharage Chande, alisema kuanza kwa biashara hiyo kutaiwezesha TANESCO kuongeza mapato yatakayosaidia kuboresha huduma mbalimbali kwa wateja wao.
“Maana ya pili tutapunguza uzalishaji wa hewa chafu ya dizeli, lakini pia kuongeza ufanisi wa kazi zao GGML kwa maana ya gharama za uzalishaji zitapungua,” alisema Chande.
Aliongeza kuwa, hatua hiyo kubwa na muhimu ya GGML kuunganishwa na umeme wa gridi ya Taifa imefikiwa baada ya miaka zaidi ya ishirini tangu kuanzishwa kwa kampuni ya GGML.
Kufanikiwa kwa jambo hilo kumetokana na jitihada mbalimbali zilizofanywa na TANESCO katika kuimarisha upatikanaji wa umeme ndani ya Mkoa wa Geita kwa kujenga kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Mpomvu chenye uwezo wa megawati 90.
Kwa upande wake Makamu wa Rais wa GGML, Simon Shayo, alisema GGML watajenga kituo cha kupokea na kupoza umeme ambazo zitatumika kwa matumizi ya mgodi.
“Kwetu sisi tunapunguza gharama za uzalishaji wa umeme tunao utumia kwa maana kwa kuacha kutumia mafuta lakini pia kutunza mazingira, Dunia sasa inatoka kwenye matumizi ya mafuta ambayo yanazalisha hewa ya ukaa," alisema Shayo.
Kampuni ya GGML kwa sasa inatumia Dola za Marekani senti 19 kuzalisha umeme kwa unit moja kwa kutumia mafuta, lakini mradi huo ukikamilika na kuunganishwa na gridi watatumia senti 9 za kimarekani kwa unit moja kupata umeme.
Mradi huo wa kupeleka umeme GGML unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu, ambapo utajumuisha njia ya kusafirisha umeme umbali wa kilometa 6 na kituo cha kupoza umeme cha GGML cha kilovolt 33.