TFF yafurahia Ushindani Kombe la FA, Watoa Pole kwa Timu zilizopigwa Bao Nyingi



SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limepongeza ubora na ushindani ulioko katika mashindano ya Kombe la FA ambayo hutoa mwakilishi wa Bara kwenye michuano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika, likisema timu nyingi kwa sasa hazifanyi mzaha kwenye michuano hiyo tofauti na zamani.

Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF, Salum Madadi, alisema pamoja na hayo, michuano hiyo msimu huu imeonyesha timu za Ligi Kuu Tanzania Bara kupiga hatua kubwa kiuwezo, ikionyesha dhahiri ubora wa ligi yenyewe.

"Kwanza nichukue fursa hii kuzipa pole timu za Daraja la Kwanza kwa kukutana na vipigo vizito, maana kuna jamaa wamepigwa nane na wengine sita, lakini nazipongeza kwa sababu mpaka kufikia pale zimefanya kazi kubwa, hivyo zisikate tamaa, " alisema Madadi.

Aliongeza kwa sasa inaonyesha Ligi Kuu Tanzania Bara ni bora sana, kwani uwezo wa timu zake unaonekana ukilinganisha na timu za chini, wakati miaka ya nyuma zilikuwa hazitofautiani sana.

"Huko nyuma timu za Ligi Kuu na madaraja ya chini zilikuwa zikizidiana kwa madaraja, lakini viwango vilikuwa havipishani sana na hata ushindani wa uwanjani ulikuwa haupishani, lakini ubora wa ligi umezifanya timu kupiga hatua kubwa, pia zinaonekana hazifanyi mzaha kwenye kombe hili," alisema.


Timu zilizobebeshwa mabao mengi kwenye michuano hiyo ya FA ni Top Boys, iliyobugizwa mabao 8-1 dhidi ya Coastal Union, huku Dar City, ikikandamizwa mabao 6-0 dhidi ya Simba kwenye hatua hiyo ya 32 bora.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad