MAKAMU Mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania cha Chadema Tundu Lissu, amemuomba Rais Samia Suluhu Hassan, alitafutie ufumbuzi suala la wabunge 19 wa viti maalumu waliofukuzwa na chama chake, akidai uwepo wao bungeni ni kinyume na katiba. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).
Lissu amesema hao jana Jumatano tarehe 16 Februari 2022, muda mfupi baada ya kumaliza mazungumzo yake na Rais Samia, jijini Brussels nchini Ubelgiji, alikokwenda kwa ajili ya ziara ya kikazi.
“Ajenda yangu ya tano ambayo nimezungumza na mheshimiwa Rais inahusu wale wabunge wa Dk. Tulia Ackson, nimemueleza Rais kwamba sisi hatuna wabunge kwenye Bunge. Wale wanaodaiwa kuwa ni wabunge wa Chadema, tulishawafukuza kwenye chama,” amesema Lissu.
Lissu amedai, Chadema ilishapeleka taarifa rasmi bungeni, kuhusu maamuzi yake ya kuwafukuza uanachama wabunge hao, hivyo kuendelea kuwepo bungeni na kupewa stahiki za kibunge, ni ufujaji wa fedha za umma.
“Tulishatoa taarifa bungeni na kwa sababu hiyo kwa mujibu wa Katiba, mtu ambaye si mwanachama wa chama cha siasa hastahili kukaa bungeni na kulipwa hela za umma kama mbunge, wakati hana sifa za kuwa mbunge,” amesema Lissu na kuongeza:
“Haijalishi kuna rufaa, suala la rufaa ni suala tofauti kabisa. Kwa sasa sio wanachama wa Chadema kuendelea kuwalipa fedha za umma ni kufanya ufujaji wa fedha za umma. Nimemwambia mheshimiwa Rais alishughulikie hili.”
Halima Mdee na wenzake 18, walitimuliwa Chadema, tarehe 27 Novemba 2020, ikiwa ni siku tatu tangu walipojipeleka bungeni na kuapishwa kuwa wabunge viti maalumu na aliyekuwa Spika wa Bunge, Job Ndugai.
Mbali na Mdee, wengine waliofukuzwa Chadema ni, Hawa Mwaifunga, Jesca Kishoa, Agnesta Lambat, Tunza Malapo, Cecilia Pareso, Asia Mwadini Mohamed, Felister Njau, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda na Kunti Majala.
Wengine ni, Ester Bulaya, Esther Matiko, Nusrat Hanje, Gace Tendega, Stella Siyao, Salome Makamba, Anatropia Theonest na Concester Lwamlaza.
Wabunge hao viti maalumu walifukuzwa Chadema wakidai kukiasi chama hicho, kufuatia kukubali kuapishwa kushika nyadhifa hizo kinyume na msimamo wake wa kutopeleka wawakilishi bungeni.