Ubadhirifu mikopo yamng’oa ofisa maendeleo



MKUU wa Wilaya ya Temeke, Jokate Mwegelo, amemtaka Mkurugezi wa Manispaa ya Temeke, kumsimamisha Ofisa wa maendeleo ya jamii kutokana na kutaka kumhamisha mtumishi aliyefichua udanganyifu katika utoaji wa mikopo.

Alitoa maelekezo hayo jana alipokuwa akipokea taarifa ya kamati aliyoiunda kwa ajili ya kufuatilia mwenendo wa utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi vya wanawake, vijana na wenye ulemavu.

Pia Jokate alimpongeza Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Elihuruma Mabelya, kwa kukataa kuuza shule kwa Sh. milioni 100.

Alisema udanganyifu si maono ya Rais kwa kuwa kulikuwa na ukakasi katika utoaji wa mikopo jambo lililosababisha kuunda kamati ya uchunguzi. Alisisitiza kuwa wale wote wanaosimama katika haki na wanaosaidia viongozi kutimiza majukumu yao kwa kusimamia haki ni lazima walindwe.

“Hatuwezi kutetea wale ambao wanasababisha kasoro na tukawaacha wale ambao wanatusaidia kazi. Chini ya uongozi wangu, sitaruhusu hilo na inawezekena hili lisiwapendeze sana lakini sidhani kwamba tuko kwenye hizi kazi kufurahishana.


 
Mwisho wa siku nitakuja kuulizwa mimi kama mkuu wa wilaya kwamba hili limetokea wewe ulikuwa wapi na ulichukua hatua zipi.

“Sasa nilisema na ninaendelea kusema kila mtu ashike hamsini zake. Kila mtu asimame kwenye wajibu wake. Uzalendo wako, uadilifu wako, mienendo yako ndiyo ikutetee kitu tunachokitaka na si vinginevyo. Tusibebeshane lawama ambazo hazistahili, tuwachukulie hatua wale wote wanaoenda kinyume cha taratibu. Lazima tuivushe wilaya yetu mahali pazuri zaidi,” alisema.

Mwenyekiti wa kamati ya ufuatiliaji mikopo hiyo, Sadath Mtwale, akiwasilisha taarifa hiyo, alisema uchunguzi ulibaini kuwa kuna baadhi ya vikundi ambavyo vilipatiwa mikopo bila kutimiza masharti yaliyoainishwa na kwamba hilo limesababishwa na baadhi ya viongozi wanaoingiza siasa katika utoaji wa mikopo hiyo.


“Baadhi ya vikundi vilivyoomba mikopo havijapitishwa katika ngazi ya kata na vikao vya baraza la kata lakini vimepitishwa katika ngazi ya manispaa na kungojea kupewa mikopo. Pia baadhi ya vikundi havijafuata utaratibu wa uombaji wa mikopo kwani kuna ambavyo vinajaziwa fomu ya uombaji wa mikopo wakati bado havijasajiliwa.

“Baadhi ya vikundi vimetengenezwa kiujanja ujanja na miongoni mwa wajumbe wake wanatoka nje ya kata husika. Pia baadhi ya watendaji wa kata wakishirikiana na maofisa maendeleo wa kata wamekuwa na tabia ya kubadilisha muhtasari wa vikao vya baraza la kata ili kuongeza majina katika vikundi ambavyo vitapatiwa mikopo,” alisema Mtware.

Alisema timu hiyo ilipitia vikundi 117 na kubaini vikundi 21 ambavyo baadhi ya wajumbe walishindwa kujitokeza mbele ya kamati na kwamba waliofika walishindwa kujibu maswali yanayohusu vikundi vyao na kuonyesha kutowajua wajumbe wenzao. Alisema hali waliyoitilia mashaka kuwa hawapo.

Pia alisema baadhi ya wanufaika ni viongozi wa manispaa hiyo ambao wamekuwa wakishiriki kutengeneza vikundi kwa ajili ya kupata mikopo kwa manufaa yao. Alisema baadhi ya fomu za utambulisho wa vikundi zimekuwa zikitiwa saini na watendaji na wenyeviti wa mitaa tofauti na ile ambayo vikundi vipo.


 
“Baadhi ya waheshimiwa wamekuwa wakiingilia utendaji wa vikundi wakilazimisha kufanyika uamuzi ambao wana maslahi nayo. Pia wamekuwa wakilazimisha kufukuzwa kwa baadhi ya wana vikundi kutokana na kuwa na misimamo ya kutokukubaliana nao.

“Baadhi ya watendaji na maofisa maendeleo wa kata wamekuwa wakipokea vitisho na mashinikizo kutoka kwa waheshimiwa au watendaji ngazi ya manispaa kutokana na misimamo yao ya kiutendaji katika utoaji wa mikopo kwa vikundi,” alidai Mtware.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad