Wakati mapigano makali yakizidi kupamba moto kwenye miji ya Kyiv, Kharkiv na Chernihiv nchini Ukraine, watu weusi wanaoishi nchini humo hususan kutoka barani Afrika wameibua madai mazito ya ubaguzi wa rangi, wakieleza kwamba baadhi ya watu weusi wamezuiliwa kuvuka mpaka wa nchi hiyo kwenda Poland kutafuta hifadhi.
Kwa mujibu wa Gazeti la The Independent la nchini Uingereza baadhi ya watu weusi wameachwa wakiwa hawajui nini cha kufanya baada ya kuzuiwa kuvuka mpaka kukimbia mapigano yanayozidi kupamba moto.
Mwanaume mmoja mweusi aliyejitambulisha kwa jina moja la Osarumen mwenye asili ya nchini Nigeria ambaye ameishi Ukraine tangu 2009, ameliambia Gazeti la The Independent kwamba yeye na wanaye watatu na mkewe, waliteremshwa kwenye basi Jumamosi wakati wakijaribu kukimbilia Poland.
Anaendelea kueleza kuwa walipohoji kwa nini wao wanateremshwa na wengine weupe wanaachwa, maafisa wa kijeshi waliwaambia kwamba ‘watu weusi hawaruhusiwi kwenye basi hilo’.