Ubalozi wa Tanzania nchini Ukraine umetoa tamko kuhusiana na hali ya sintofahamu ya kiusalama inayoendelea nchini humo.
Taarifa iliyotolewa na Ubalozi wa Tanzania nchini humo, imeshauri kuwa wote wanaodhani kukaa Ukraine kwa sasa sio salama waondoke nchini humo.
Aidha kwa wazazi wenye watoto wanaosoma nchini humo na wanataka watoto wao warejee kwa muda hadi hapo uvumi wa kutokea vita utakapoisha, wafanye utaratibu binafsi wa kuwarudisha watoto wao nyumbani kwa kutumia ndege za abiria zinazofanya safari kutokea Ukraine.
Pia ubalozi umeshauri wanafunzi wanaotaka kurudi nyumbani wawasiliane na uongozi wa vyuo wanavyosoma na kukubalina kuendelea kwa masomo kwa njia ya mtandao (Online) kipindi chote watakachokuwa nje ya Ukraine.