Askari wa Ukraine akiwa eneo la mapigago kati yao na Russia jijini Kyiv. Picha na AFP
Tangu Russia ilipoivamia Ukraine mapema wiki hii, mapambano ya majeshi ya nchi hizo mbili yanaendelea na mpaka jana mapigano yalikuwa yamefika katika mitaa ya Jiji la Kyiv.
Katika majibizano hayo, vikosi vya majeshi ya Ukraine vilizuia shambulio la Russia, ingawa “makundi ya hujuma” yaliingia katika mji mkuu, maofisa walisema jana huku Rais Volodymyr Zelensky akiapa kuwa Ukraine haitakubali kamwe.
Katika siku ya tatu ya uvamizi ambao umesababisha vifo vya raia 198, wakiwamo watoto, Russia imeendelea kupuuza msururu wa vikwazo inavyowekewa na nchi za magharibi, hivyo kuendelea kurusha makombora kuyalenga maeneo ya jeshi la Ukraine.
“Nipo hapa. Hatutaweka chini silaha yoyote, tutaitetea Serikali yetu kwa sababu silaha zetu ni ukweli wetu na ukweli ni kwamba hii ni ardhi yetu, nchi yetu, watoto wetu na tutayalinda haya yote,” alisema Rais Zelensky.
Uvamizi wa Russia umeshasababisha makumi ya maelfu ya wananchi kuyakimbia makazi yao, huku Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron akionya dunia kujiandaa kwa vita ndefu.
“Mgogoro huu utadumu, vita hivi vitadumu na machafuko yote yanayoambatana navyo yatakuwa na matokeo ya kudumu. Lazima tujitayarishe,” alisema Macron.
Wizara ya Ulinzi nchini Ukraine ilisema “helikopta mbili za maadui aina ya SU-25 zilidunguliwa karibu na eneo linalotaka kujitenga mashariki mwa nchi hiyo.”
Taarifa hiyo ilifafanua kuwa ndege ya kijeshi ya mizigo ya Russia aina ya Ilyushin Il-76 pia imeangushwa huko Vasylkiv, kilomita 30 kusini magharibi mwa Kyiv.
Bila kutoa ushahidi, Msaidizi wa Rais wa Ukraine, Mykhailo Podolyak alisema zaidi ya wanajeshi 3,500 wa Russia wameuawa na kuwakamata 200.
Hata hivyo, taarifa iliyotolewa na ikulu ya Kremlin mjini Moscow jana iliishutumu Ukraine kwa kuendeleza mzozo huo wa kijeshi kwa kukataa kufanya mazungumzo, lakini ikaendelea kuivamia nchi hiyo inayoungwa mkono na mataifa ya magharibi.
“Kuhusiana na mazungumzo yaliyotarajiwa, Rais wa Russia jana alasiri aliamuru kusimamishwa kwa mashambulizi yanayofanywa na vikosi vya jeshi letu, lakini Ukraine imekataa kufanya mazungumzo hayo, hivyo vikosi vikaendelea kuishambulia Ukraine kuanzia mchana huu,” alisema msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov alipozungumza na waandishi wa habari.
Juzi Ijumaa, wakati vikosi vya Moscow vili-polikaribia Jiji la Kyiv, ikulu ya Russia ilise-ma Rais Putin alikuwa tayari kutuma ujumbe wa mazungumzo huko Belarusi, ambapo Russia imeweka maelfu ya wanajeshi.
Upande huo ni mojawapo ya maeneo ambayo Ukraine inasema inashambuliwa zaidi. Saa chache baadaye, Putin alitoa wito kwa Jeshi la Ukraine kuupindua uongozi wa nchi hiyo alioutaja kama unaoongozwa na ma-gaidi na genge la waraibu wa dawa za kulevya na Wanazi mamboleo.
Kwa upande wake, Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine ametoa wito mara kwa mara wa mazungumzo na kiongozi huyo wa Russia wakati wa msukumo wa kidiplomasia wa wiki nzima ambapo nchi za magharibi zilijaribu kumzuia Putin kuishambulia nchi yake.
Wakati wanajeshi wa Urusi walipokaribia Kyiv juzi Ijumaa, Zelensky alitoa taarifa mpya akihimiza mazungumzo ya kusitisha mapigano.
“Ningependa kumwambia Rais wa Shirikisho la Russia kwa mara nyingine, tuzungumze. Mapigano yanaendelea kote nchini Ukraine. Tuketi kwenye meza ya mazungumzo ili kukomesha vifo vya watu,” alisema.
Jana Russia ilisema “imejiandaa kwa umakini kwa vikwazo vya kimataifa ambavyo imevitabiri.”
Nguvu iliyopotea
Hadi mwaka 1991 Ukraine ilikuwa nchi ya tatu kwa hifadhi kubwa ya silaha za nyuklia duniani, lakini walioishawishi kuachana na hifadhi ya silaha hizo ndio wameivamia na kuipiga sasa hivi.
Baada ya kuanguka kwa Jamhuri ya Muungano wa Kisovieti (USSR) mwaka 1991, ilikuwa nchi huru kuanzia Agosti 24 ilipojitangazia kujitawala na Desemba mosi wananchi walipiga kura ya maoni kuurasimisha uhuru wao. Zaidi ya asilimia 90 waliukubali uhuru huo, wakiwamo asilimia 56 kutoka Jimbo la Crimea.
Kuanzia Desemba 26 mwaka 1991, USSR ilivunjika rasmi wakati marais wa Ukraine, Belarus na Russia ambazo ni wanachama waanzilishi walipokutana katika Msitu wa Bialowieza. Kuanzia hapo, uhuru wa Ukraine ulitambuliwa na jumuiya ya kimataifa.
Kuvunjika kwa umoja huo kuliilazimu iliyokuwa Serikali ya USSR kuacha maelfu ya silaha za nyuklia katika ardhi ya Ukraine ambayo miaka kadhaa mbele iliamua kuachana nazo kabisa.
Kwa kubadilishana, Marekani, Uingereza na Urusi zilitoa dhamana ya usalama kwa Ukraine katika makubaliano ya Desemba 5 mwaka 1994 yanayojulikana kama Mkataba wa Budapest kuwa itakuwa salama iwapo itaachana na silaha za nyuklia.
Mwaka 2009, Russia na Marekani zilitoa taarifa ya pamoja kwamba mkataba huo wa usalama ungeendelea kuheshimiwa, lakini hata kabla ya kuvamiwa na Russia, Ukraine ilianza kuwa na wasiwasi kuwa mkataba huo hauheshimiwi tena kutokana na vitisho ilivyokuwa inapewa na Russia.
Wakati wa kusaini mkataba huo na miaka kadhaa baadaye, Ukraine iliambiwa na Marekani na nchi za magharibi, ikiwamo Uingereza kwamba wanachukua dhamana za kisiasa kwa uzito kwa ajili ya usalama wa Ukraine kwa sababu hati hiyo ilisainiwa na viongozi waandamizi wa nchi zilizohusika.
Kilikuwa ni kiapo chao kwamba Ukraine haitaachwa isimame peke yake kukabiliana na tishio lolote ikiwa ingeshambuliwa.
Kwa muda mrefu, Ukraine ilikuwa na imani kwamba nchi za magharibi pamoja na Russia wakati wote zingesimama upande wake ingawa haikuwa na uhakika sana na Russia.
Russia yakiuka mkataba
Kwa kuwa dalili zilianza kuonekana mapema, mkataba ulikuwa na kipengele kinachoruhusu mashauriano iwapo kutakuwa na suala litakalohitaji kufanya hivyo.
Machi 4, Ijumaa ya mwaka 2014 ulifanyika mkutano ulioitishwa na Ukraine jijini Paris, Ufaransa lakini Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergey Lavrov ambaye alikuwa Paris wakati huo, hakutokea.
Kwenye majibu yake, Russia ilisema ilitia saini na serikali tofauti, si iliyokuwapo wakati huo ambayo yenyewe ilikuwa inaiona kuwa haramu. Alipoulizwa Lavrov alisema: “Husaini mkataba na serikali, unasaini na nchi.”
Inawezekana Ukraine sasa inajutia kitendo chake cha kusainishwa hati ya usalama ili kuachana na silaha za nyuklia, kwani madhara yangekuwa madogo kiuchumi hata katika siasa za kimataifa iwapo ingeshikilia msimamo wake, kwani Russia leo wangelazimika kufikiria mara nyingi kabla ya kuishambulia.
Katika nyanja za umma, simulizi hizi zina mashiko. Ukraine walikuwa na ghala la tatu la silaha za nyuklia kwa ukubwa duniani, lakini hati hiyo ya uhakikisho wa usalama ilipendekeza kuiondolea nguvu hiyo ambayo ingekuwa muhimu kipindi hiki inaposhambuliwa.
Ikiwa na karatasi ya mkataba huo, hivi sasa Ukraine siyo tishio kwa Russia, ndiyo maana imekuwa rahisi kuvamiwa na maswahiba iliowategemea kuitetea bado hawajachukua hatua zinazoweza kuisaidia kuendesha mapambano hayo.
Majuto yanatokana na uamuzi wa kizembe wa kukubali kupokonywa silaha zao kisha kugeuzwa shabaha ya tishio kama hilo kubwa mikononi mwa nchi yenye silaha za nyuklia.
Hata hivyo, wachambuzi wanasema ukweli huu unatoa ujumbe kwa nchi nyingine nazo kuwa na silaha za nyuklia ili zisitishwe na yeyote au ziweze kujibu mashambulizi pale itakapobidi.
Hata hivyo, Ukraine ilifanya jambo sahihi wakati huo. Ilikuwa sahihi kwake yenyewe na mbele ya jumuiya ya kimataifa kwa kuwa mfano kuchangia kupunguza idadi ya silaha za nyuklia ulimwenguni ili kila mtu awe salama.
Kwa historia hii, wadhamini waliotia saini Mkataba wa Budapest na jumuiya ya kimataifa kwa upana wake wanahitaji kuguswa kwa njia ambayo haitaifanya Ukraine kuwa na shaka katika usahihi wa uamuzi wa kuachana na silaha za nyuklia.
Huenda kinachoisikitisha Ukraine ni kuwa mojawapo ya nchi zilizoishawishi kuachana na silaha za nyuklia na kutia saini hati ya uhakikisho wa usalama dhidi ya taifa lolote litakaloishambulia ndiyo hiyo ambayo sasa imeishambulia, na zile nchi nyingine kama Marekani na Uingereza ambazo nazo ziliishawishi kusaini hati hiyo, hazijaisaidia kipindi hiki inaposhambuliwa.
Anaowasikiliza Putin
Rais wa Vladmir Putin wa Russia anao marafiki wengi ambao ni matajiri anaowasikiliza kiasi cha kuufanyia kazi ushauri wanaompa. Marafiki hawa ni wa ndani na nje ya Taifa lake ambalo nguvu zake za kijeshi zinaiyumbisha dunia hivi sasa.
Kwenye orodha hiyo, yumo Igor Sechin, ofisa wa Serikali ya Russia anayechukuliwa kuwa mshirika wa karibu, akihudumu kama Naibu Rais. Ni mkuu wa kampuni kubwa ya mafuta duniani. Sechin ni mmoja wa watu wenye nguvu zaidi nchini Russia.
Hata hivyo, Alhamisi iliyopita Marekani imemwekea Sechin vikwazo baada ya Russia kuivamia Ukraine. Sechin mara nyingi huelezewa kama mmoja wa washauri wa kihafidhina zaidi wa Putin na kiongozi wa kikundi cha Siloviki cha Kremlin ambacho ni mkusanyiko wa mawakala wa zamani wa huduma za usalama.
Hadi Mei 21 mwaka 2012, alihudumu kama Naibu Waziri Mkuu wa Russia katika baraza la mawaziri la Putin na kwa sasa ni ofisa mkuu mtendaji, rais na mwenyekiti wa bodi ya usimamizi ya Rosneft, kampuni ya mafuta ya Serikali nchini Russia.
Mwingine ni Gennady Timchenko, mmoja wa waanzilishi wa Gunvor, kampuni ya kimataifa ya mafuta na nishati duniani. Yeye ni mfanyabiashara na mjasiriamali bilionea.
Alianzisha na kuimiliki Volga Group, kampuni ya uwekezaji inayojielekeza katika sekta ya nishati, usafirishaji na miundombinu. Hapo awali alikuwa mmiliki mwenza wa Gunvor Group. Hadi Aprili 15 mwaka 2021, Timchenko aliorodheshwa katika nafasi ya 96 ya mabilionea na gazeti la Bloomberg, akikakadiriwa kuwa na utajiri wa dola 19.5 bilioni za Marekani, hivyo kumfanya kuwa mtu wa sita tajiri zaidi nchini Russia. Vilevile, ni balozi wa heshima wa Serbia huko Saint Petersburg.
Rafiki mwingine anayeshibana na Rais Putin nchini Russia ni Dmitry Medvedev, mwanasiasa anayehudumu kama naibu mwenyekiti wa Baraza la Usalama la Russia tangu mwaka 2020. Alikuwa Rais tangu 2008 hadi 2012 na waziri mkuu kuanzia mwaka 2012 hadi 2020.
Dmitry Medvedev na Putin wana historia ndefu. Wote wawili wanatoka St Petersburg na walifanya kazi chini ya Meya Anatoly Sobchak miaka ya 1990. Baada ya Putin kuhamia Moscow na kuwa waziri mkuu, Medvedev alichaguliwa kuwa Rais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2008.
Ajenda kuu ya Medvedev akiwa Rais ilikuwa mpango mpana wa kisasa unaolenga kufanya uchumi wa Russia na jamii kuwa wa kisasa na kupunguza utegemezi wa nchi hiyo kwa mafuta na gesi. Kutokana na historia yao ya muda mrefu, Medvedev anatajwa kuwa mtu wa karibu zaidi wa Rais Putin.
Vilevile, yupo Kirill Shamalov ambaye ni mkwe wa Vladimir Putin. Shamalov amemuoa binti wa Putin anayeitwa Katerina. Shamalov ni mtoto wa Nikolai Shamalov, rafiki wa zamani wa Putin kutoka St Petersburg. Aprili 2018, Marekani ilimwekea vikwazo yeye na raia wengine 23 wa Russia.
Kuanzia Februari 2013 alipofunga ndoa na Katerina, alijiunga na kikundi cha mabilionea wasomi walio karibu na Rais Putin. Shamalov amekuwa mbia mkuu wa Sibur na ndani ya miezi 18 baadaye alipokea mkopo wa dola bilioni kutoka Gazprombank, benki iliyowekewa vikwazo vya Marekani.
Pamoja na yote yanayoendelea, Shamalov anatajwa kuwa miongoni mwa watu wanaosikilizwa sana na Rais Putin, kwani ni mtu wake wa karibu anayeweza kumshauri mambo muhimu kwa mustakabali wa Taifa hilo kubwa kijeshi na kiuchumi.
Mtu mwingine mwenye uwezo wa kumsogelea Rais Putin na kumweleza lolote lililo moyoni mwake ni Sergei Roldugin, mwigizaji katika Jiji la St Petersburg. Yeye ndiye aliwezesha Putin afahamiane na Lyudmila Ocheretnaya ambaye ni mama wa binti mkubwa wa Putin, Maria.
Roldugin ni baba wa ubatizo wa Maria ambaye ni binti mkubwa wa Vladimir Putin. Yeye na Putin wamekuwa marafiki tangu mwishoni mwa miaka ya 1970. Machi 2016 baadhi ya vyombo vya habari nchini Uingereza vilimtaja Roldugin kama “rafiki mkubwa wa Putin.”
Yeye ni mfanyabiashara nchini Russia akiishi katika Jiji la St Petersburg. Kila inapobidi anaweza kukutana na Rais wake huyo wakazungumza kwa kina.
Nje ya Russia mtu mwenye nafasi kubwa ya kusikilizwa na Rais Putin ni Kansela wa zamani wa Ujerumani, Gerhard Schroder. Kansela huyo tayari ameishutumu Ukraine kwa kuropoka katika mzozo kati yake na Russia.
Hii si mara ya kwanza kuonekana akimtetea rafiki yake, Rais Vladimir Putin. Viongozi hawa wamekuwa wakitembeleana. Inaaminika Shroder ndiye mwanasiasa namba moja nje ya Russia anayesikilizwa zaidi na Putin.