Urusi Yakumbana na Upinzani Mkali Ukraine, Wanajeshi Warudi Nyuma Kujipanga Upya


Wakati mapigano kati ya majeshi ya Urusi na Ukraine yakiingia siku ya nne, taarifa zinaeleza kwamba Urusi imekumbana na upinzani mkali ambao haikuutegemea kutoka kwa majeshi ya Ukraine huku idadi ya vifo kwa pande zote mbili ikizidi kuongezeka.

Taarifa za wachambuzi wa masuala ya kivita, zinaeleza kwamba Urusi ilitegemea kuuteka Mji Mkuu wa Kyiv kirahisi ndani ya muda mfupi lakini hali inayoendelea kwa sasa inaonesha kwamba majeshi ya Ukraine yanaendelea kupambana vikali kuhakikisha kwamba mji huo hauangukii kwenye mikono ya majeshi ya Urusi na tayari yamefanikiwa kuyarudisha nyuma majeshi ya Urusi.

Taarifa zaidi zinaeleza kwamba mpaka sasa, Urusi imefanikiwa kwa asilimia 50 katika uvamizi huo uliohusisha wanajeshi takribani 150,000 wa Urusi wakiwa na silaha nzito ambapo kutokana na upinzani iliokutana nao kutoka kwa wanajeshi wa Ukraine, huenda ikaongeza idadi ya wanajeshi katika siku chache zijazo.

Mchambuzi Nigel Gould-Davies kutoka Chuo cha International Institute for Strategic Studies kilichopo jijini London, Uingereza ambaye pia amewahi kuwa Balozi wa Uingereza nchini Belarus, amenukuliwa akisema Urusi imekutana na kikwazo kikubwa kutoka kwa Jeshi la Ukraine ambapo mpaka sasa, maafisa kadhaa wa ngazi za juu wa Jeshi la Urusi, wakiwemo mabrigedia wawili wametekwa na wanajeshi wa Ukraine.

Naye Tom Bullock, mchambuzi wa taarifa za Kiintelijensia kutoka Kampuni ya Janes, amenukuliwa akisema mpaka sasa Urusi imeshindwa kutumia ukubwa wa jeshi lake na nguvu za kivita kulikamata Jiji la Kyiv ndani ya muda mfupi kama ilivyotarajiwa na wengi na kueleza kwamba hata katika miji mingine mbali na Kyiv, wanajeshi wa Ukraine wameendelea kufanya kazi kubwa ya kuwarudisha nyuma wanajeshi wa Urusi.


Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad