Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel akizungumza baada ya kushiriki kwenye kampeni ya usafi wa mazingira jijini Dodoma
Dodoma. Watu watatu wamefariki dunia ndani ya mwazi Februari mwaka huu kutokana na ugonjwa wa Uviko-19.
Hayo yamesemwa leo Februari 10 na Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel wakati akishiriki usafi katika soko la Mavunde, Chang'ombe jijini Dodoma ambapo amesema idadi vifo hivyo ni kwa nchi nzima ndani ya mwezi huu.
Dk Mollel alikuwa kwenye kampeni ya usafi wa mazingira inayoratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira na leo ni zamu ya usafi katika masoko.
Amesema kuwa watu hao waliofariki hawakuwa wamechanja huku akibainisha kuwa wengi waliochanja wamekuwa wakiugua ugonjwa huo lakini hauwasumbui kama inavyokuwa kwa ambao hawajachanja.
Naibu Waziri huyo aliongeza kuwa Uviko-19 ni moja ya magonjwa ya mlipuko ambayo yanasababishwa wakati mwingine na uchafuzi wa mazingira, hivyo kufanya usafi ni sehemu ya kuepuka magonjwa na kuchanja ndiyo suluhu ya kuukimbia Uviko-19.
“Si mnajua mojawapo ya wabishi wa kuchanja tulikuwa sisi, lakini tumejiridhisha na Rais amesema chanjo ni salama, sasa twendeni tukachanje ndugu zangu,” amesema Dk Mollel.
Akizungumzia usafi wa mazingira, ametaka sheria za Jiji kuwabana wananchi katika usafi na upandaji miti kama wanavyobanwa kwenye suala la kuezeka mabati ya rangi katika nyumba zao.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mzingira, Mary Maganga amesema kampeni ya kupanda miti inakwenda sambamba na usafi wa mazingira nchi nzima.
Mwananchi