WAKILI, Mosses Mahuna amedai mahakamani kuwa, Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha ilikosea kuamini kuwa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya (35) na wenzake wawili walikuwa wanamiliki genge la uhalifu.
Mahuna anayemtetea Ole Sabaya (35) na wenzake wawili amedai kuwa, ushahidi haukutosha kuthibitisha washtakiwa hao walitenda kosa la unyang'anyi wa kutumia silaha na kuwafunga miaka 30 jela.
Alisema hayo mbele ya Jaji Sadekia Kisanya wakati akiwasilisha sababu za rufaa za kutaka Sabaya, Silvester Nyengu (26) na Daniel Mbura (38) waachiwe huru.
Mahuna alidai Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha ilipaswa kuwaachia huru washtakiwa hao kwa kuwa mashahidi upande wa Jamhuri hawakuthibitisha mashitaka dhidi yao.
Alidai badala ya mahakama kuamini kuwa Sabaya na wenzake walikuwa wakimiliki genge la uhalifu, ilipaswa kujielekeza katika shitaka la unyang'anyi wa kutumia silaha kwa kuwa mashahidi hawakuthibitisha shitaka hilo hivyo wateja wake wanastahili kuachiwa huru.
Mahuna pia alidai hakukuwa na gwaride la utambuzi kwa wakata rufaa na kama lilifanyika halikuzingatia sheria 13 za PGO ya Polisi na kilichofanyika ni kiini macho.
Alidai shahidi namba sita wa upande wa Jamhuri, Bakari Msangi alikuwa akifahamiana na mleta maombi wa kwanza wa rufaa hiyo, lakini maelezo yake polisi aliyoyatoa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha yanatofautiana, hivyo akamuomba Jaji Kisanya atoe uamuzi kwa kuzingatia hilo.
Mahuna alisema Msangi alidai mahakamani kuwa alimwona mleta rufaa wa pili katika eneo la tukio Februari 9, mwaka jana, lakini katika maelezo yake polisi hakumtaja hivyo huo ni utata.
Pia alidai Msangi alimtambua mleta rufaa wa kwanza, Andrew na Deogratus Peter kuwa walikuwepo katika eneo la tukio, lakini hakumtaja mleta maombi wa tatu hivyo inatia shaka kama alikuwa mwaminifu katika kutoa ushahidi.
Mahuna aliendelea kudai kuwa, Msangi alidai alipofika dukani siku ya tukio na kuingia ndani alimtambua mleta maombi wa kwanza na wa pili, lakini shahidi wa tatu na wa nne upande wa Jamhuri hawakusema kama mleta maombi wa kwanza na wa pili wa rufaa walikuwepo siku hiyo, hivyo Jaji pia azingatie hilo.
Alidai Msangi hapaswi kuaminiwa katika ushahidi alioutoa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha kwa kuwatambua mleta maombi wa pili na wa tatu kwa sababu maelezo yake yanatofautiana na aliyoyatoa katika Kituo Kikuu cha Polisi Arusha.
Upande wa utetezi jana ulimaliza kuwasilisha hoja zao na mahakama ilikubali ombi la upande wa Jamhuri kuomba siku moja wapitie hoja za wakata rufaa hivyo kesi hiyo itaendelea kesho.