Wanachama 204 waliokimbia CUF warejea



Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi CUF, Profesa Ibrahim Lipumba akiongoza mapokezi ya wanachama wanachama 204 waliorejea kwenye chama hicho leo Jumapili Februari 20, 2022.
Dar es Salaam. Chama Cha Wananchi (CUF) kimewapokea wanachama 204 waliorudi wakitokea vyama vingine.

Miongoni mwa wanachama hao waliotambulishwa kutoka CCM, Chadema na ACT Wazalendo, 133 ni kutoka Tanzania Bara na 71 kutoka visiwani Zanzibar.

Akizungumza leo Jumapili Februari 20, 2022 katika hafla ya kuwakaribisha wananchama hao iliyofanyika Makao makuu ya chama hicho Buguruni jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahimu Lipumba amesema watapangiwa majukumu ya kukijenga chama hicho.

“Nawashukuru kwa kurudi nyumbani sehemu ambayo haki inapiganiwa na nitoe wito kwa wengine warejee CUF, waje washike nafasi za uongozi hasa Zanzibar.


 
“Wengine hasa mimi umri wangu umeshakwenda, tunahitaji vijana waje waunganishe nguvu kuendelea mapambano ya kupigania haki sawa kwa wote,” amesema Profesa Lipumba.

Amesema chama hicho kinahitaji vijana kuziba nafasi mbalimbali kuelekea kwenye uchaguzi mkuu wa 2025 na kudai tume huru na Katiba mpya.

Akizungumza kwaniaba ya wale wanachama waliorejea, Masoud Hamad Masoud ameushukuru uongozi wa CUF kwa kuwaandalia mapokezi makubwa.


Masoud aliyegombea uenyekiti ACT Wazalendo mwaka huu, kabla ya kujitoa kwenye chama hicho, amesema sababu ya kurudi CUF ni kuandamwa na makada wa chama hicho tangu alipotangaza nia ya kugombea wadhifa huo ambao Juma Haji Duni alishinda.

"Kama kungelikuwa na uchaguzi huru, haki na demokrasia ningemshinda Duni na asingepata hata asilimia 20.

"Waliona Hamad akiwa mwenyekiti ni mwiba walifanya mambo mengi wanayoyajua ikiwemo Kamati yote ilikuwa inanipinga. Nafikiri Mimi hata kama ningeshinda nisingeweza kufanya Kazi peke yangu kwa sababu kamati yote ilikuwa hainiungi mkono," amesema.

Masoud katika maelezo yake ameeleza si kwamba kukosa uwenyekiti  ndani ya ACT kumemfanya kurudi CUF, isipokuwa  hana uroho wa madaraka kwani amewahi kushika nafasi kubwa serikalini lakini alijiuzulu kwa lengo la kulinda maslahi ya wananchi.

"Niliwahi kuwa Waziri wa Miundombinu na Uchukuzi Zanzibar nilijiuzulu kwa sababu meli ilizama na iliua watu wengi, sikuwa kepteni wala nahodha. Nilijiuzulu kwa lengo la kulinda heshima na chama changu hata uchaguzi ule sikuona haki pale," amesema.

Masoud ameitaka ACT Wazalendo kurudisha ofisi zote wanazofanyia Zanzibar kwa kuwa ofisi hizo zilijengwa kwa michango ya wananchama wa CUF.

“Nyaraka kila kitu kipo nategemea watazirudisha haraka sana na tunatoa muda wa wiki moja wafanye hivyo na tunajua Zanzibar wanaofisi mbili tu tunalifuatilia suala hili,” amesema.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad