Katibu wa NEC Oganaizesheni, Dk Maudline Castico akitoa taarifa ya majumuisho ya mchakato wa kuchukua na kurudisha fomu za kuomba ridhaa ya kuchaguliwa kugombea nafasi ya Naibu Spika kupitia chama cha Mapinduzi (CCM) jijini Dodoma.
Dodoma. Wabunge 11 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamechukua na kurejesha fomu za kuomba kuteuliwa kukiwakilisha chama hicho kugombea nafasi ya Naibu Spika wa Bunge la Tanzania.
Fomu hizo zilizochukuliwa kwenye Ofisi za makao Makuu ya chama hicho Dodoma, Ofisi ndogo Dar es Salaam na Afisi kuu Zanzibar zimechukuliwa kwa siku tatu kuanzia Februari 4 mwaka huu.
Akitoa taarifa ya majumuisho kwa waandishi wa habari leo Jumapili Februari 6, 2022 Katibu wa NEC Oganaizesheni, Dk Maudline Castico amesema wote waliochukua fomu hizo wamerejesha.
Amesema waliochukua na kurejesha fomu hizo ni Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kusini-Iringa, David Kihenzile, Mbunge wa Mahonda Mkoa wa Kaskazini- Zanzibar, Abdullah Ally Mwinyi na Mbunge Nzega vijijini- Tabora, Dk Hamisi Kigwangala.
Wengine ni Mbunge Jimbo la Ilala Mussa Zungu, Mbunge wa Hanang Mhandisi Samwel Hhayuma Xaday, Mbunge Muleba Kusini Dk Oscar Kikoyo na Mbunge wa Mwanga, Anania Thadayo.
Wabunge wengine waliorejesha fomu hizo ni; Mbunge wa Korogwe Vijijini Timetheo Mnzava, Mbunge wa Kilombero Abubakar Asenga, Kirumbe Ng'enda kutoka Kigoma Mjini na Mbunge wa Maswa Mashariki, Stanslaus Nyongo.
"Kufuatia mchakato huu kumalizika ratiba ya vikao vya Kitaifa vya Chama Cha Mapinduzi ambavyo vitaanza na Kamati maalumu ya Halmashauri Kuu ya Zanzibar, Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM vitaendelea" amesema.
Mchakato huo umekuja baada ya aliyekuwa Naibu Spika Dk Tulia Ackson kuchaguliwa kuwa Spika wa Bunge kuchukua nafasi iliyoacha na aliyekuwa Spika Job Ndugai ambaye alijiuzulu Januari 06 2022.