Watumishi NHIF wasomewa kesi ya makosa 811
OFISI ya Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Serikali (DPP) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Mara imeondoa mahakamani kesi Na. 23 ya mwaka 2021 iliyokuwa na makosa 30 dhidi ya wafanyakazi 11 wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na kuwafungulia kesi yenye makosa 811.
Wakili wa Ofisi ya DPP, Tawabu Issa alieleza hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma, Eugenia Rujwahuka kuwa DPP alitumia Kifungu cha 91 (i) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Sura ya 20 na marejeo ya Mwaka 2019.
Baada ya hoja hiyo kuridhiwa, Wakili huyo aliomba kuwasomea washtakiwa wote Mashtaka Sita, yenye jumla ya makosa 811 katika kesi ya Uhujumu Uchumi Na. 01/2022 ambayo ilisajiliwa mahakamani hapo juzi.
Alitaja majina, vyeo au vilivyokuwa vyeo vyao na vituo vya kazi ndani ya NHIF kuwa ni Mhasibu Msaidizi – Mara, Francs Mchaki (37) akiwa ni mshtakiwa kwa kwanza, wa pili, Msimamizi – Mara, Dk Leonard Mitti (51), wa tatu ni Meneja –Mara, Dk Mgude Bachunya (51) na wa nne ni Mhasibu Msaidizi – Mara, Jesca Mataba (28).
Alisema wa tano ni Mhasibu Mkuu - Dar es Salaam, Grace Godi (43), wa sita ni Mkaguzi Mkuu wa ndani – Dar es Salaam, Anne Maneno, wa saba ni Ofisa madai – Dar es Salaam, Myriam Fungameza (50) wa nane ni Mhasibu Mkuu – Dar es Salaam, Goodluck Kirabe (37) na wa tisa ni Mkurugenzi wa Uendeshaji na Uwekezaji – Dar es Salaam, Deusdedit Rutazaa, wa 10 ni Julius Mziray (41) na wa 11 ni Zakayo Mampagwa wote Wakaguzi wa Ndani – Dar es Salaam.
Kutokana na wingi wa makosa, hakimu alitaka upande wa Jamhuri kusoma maelezo ya awali ya shtaka la kwanza na la 811 yanayowahusisha washtakiwa wote na pia nakala za hati hiyo zitolewe kwa kila mshtakiwa na kwa Mahakama hiyo. Wakili Issa alisema washtakiwa wote wanahusishwa na kosa la kuongoza genge la uhalifu kwa lengo la kujipatia Sh 3,003,879,686 mali ya NHIF.
Alisema katika tarehe na maeneo tofauti kati ya 13 Mei, 2013 na 30 Machi, 2016 jijini Dar es Salaam na mkoani Mara wakiwa waajiriwa wa NHIF waliongoza genge la uhalifu na kujipatia kiasi hicho cha fedha kinyume cha sheria.
Kosa la 811 linawahusisha washtakiwa wote kwamba katika tarehe na maeneo tofauti kati ya 13 Mei, 2013 na 30 Machi, 2016 jijini Dar es Salaam na mkoani Mara kwa makusudi walisababishia NHIF hasara ya zaidi ya Sh bilioni 3.3.
Washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kufuatia mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.
Wakili aliomba mahakama tarehe nyingine ya kesi hiyo kutajwa kwasababu upelelezi haujakamilika, ilipangwa Machi 10, mwaka huu.
Washtakiwa wote walipelekwa rumande wakiwamo washtakiwa wa kwanza hadi wa tatu ambao awali walikuwa nje kwa dhamana, lakini mabadiliko hayo yalisababisha dhamana yao kufutwa mpaka taratibu zitakapofuatwa katika Mahakama Kuu ya Kanda Musoma.