Waziri wa Katiba na Sheria George Simbachawene, ametaka watumishi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kuanza kuchunguza na kuyachukulia hatua baadhi ya makampuni ya simu za mkononi na watumishi wake ambao wanatoa taarifa za miamala ya wateja wao kwa wahalifu wa mitandaoni.
Waziri Simbachawene ametoa rai hiyo wakati akifungua mafunzo ya makosa ya kimtandao kwa mawakili wa serikali, ambapo amesema inashangaza kuona baadhi ya wahalifu wa kimtandao kuwa na taarifa za mteja aliyefanya muamala wa simu bila kushirikiana na baadhi ya watumishi wa kampuni hizo na kuagiza watakaobainika kuchukuliwa hatua.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mashtaka DPP Sylvester Mwakitalu, amesema kuwa baada ya mafunzo hayo wanaimani mawakili wa serikali watafanyakazi kwa weledi katika kushughulikia makosa ya kimtandao na kuondoa malalamiko mengi ambayo yamekuwa yakielekezwa kwao kutokana na vitendo hivyo kuonekana kuongezeka siku hadi siku.