Wizi wa mafuta sasa watishia mradi SGR



VITENDO vya wizi wa mafuta ya magari na mitambo mingine katika  mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), vinatishia kurudisha nyuma juhudi za serikali kukamilisha miradi ya kimkakati kwa wakati.

Tuhuma za wizi huo wa mafuta ziliibuliwa na Mkuu wa Wilaya ya  Shinyanga,  Jasinta Mboneko, mwishoni mwa wiki alipofanya ziara ya kutembelea mradi huo.

Mboneko alisema ikiwa wizi huo utaendelea, atawafukuza kazi madereva wote wanaofanyakazi hapo na kupeleka vijana wengine wenye uzalendo.

Alisema madereva hao  wamekuwa na tabia ya kuiba mafuta na kuyahifadhi kwenye makazi ya watu, kitendo ambacho kinahujumu mradi huo.

Mboneko alifanya ziara hiyo ili  kuona maendeleo ya ujenzi wa mradi huo pamoja na kuzungumza na wananchi na wafanyakazi katika eneo hilo.


 
Alisema anasikitishwa kuona madereva wanaiba mafuta na kushindwa kuwa wazalendo katika nchi yao badala yake wanaipa hasara serikali.

“Madereva ambao mmepata ajira kwenye mradi huu  wa ujenzi wa SGR,  kipande hiki cha tano sijapendezwa na tabia yenu mmekithiri sana kwa wizi wa mafuta na hivi karibuni tulikamata madumu 37 ya mafuta yakiwa yamefichwa kwenye makazi ya wananchi, acheni tabia hiyo mara moja huko ni kuhujumu mradi huu,”  alisema Mboneko.

Aidha,  alisema kitendo cha kuficha mafuta kwenye makazi ya wananchi ni hatari utakapotokea moto kuwaka katika makazi yao.


Katika hatua nyingine, Mboneko alisema suala la malalamiko yao juu ya mikataba mibovu atalifanyia kazi na tayari ameshatoa maagizo kwa naibu meneja wa mradi huo kipande hicho cha tano.

Aliwatoa wasiwasi wananchi ambao mradi huo umepita kwenye mashamba yao na makazi kwamba kila mtu atalipwa fidia kwa mujibu wa sheria.

Ofisa operesheni kutoka Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani Shinyanga, Inspekta Edward Lukuba, alisema kitendo ambacho wanakifanya madereva hao kuhifadhi mafuta  kwenye makazi ya watu ni hatari ikitokea ajali ya moto.

Naibu meneja wa mradi huo,  Alex  Bunzu, alisema maagizo yote yaliyotolewa kwao atayatekeleza likiwamo suala hilo la ulipwaji wa fidia na utoaji wa mikataba kwa wafanyakazi.

Aliwataka vijana  wanaofanyakazi katika mradi huo kuwa wazalendo na nchi yao na kuacha tabia ya wizi wa vitu mbalimbali.

Akizungumzia ujenzi wa mradi huo, alisema umefikia asilimia 4.5  na utakamilika  mwaka 2024 kwa gharama ya Sh. trilioni 3.

Baadhi ya madereva hao walisema wapo wanaojihusisha na wizi huo wa mafuta kutokana na malipo kuwa kidogo  ambayo ni Sh.12,500 kwa siku.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad