Yanga Waongezewa Dau Maradufu



YANGA ambayo jana usiku ilikiwasha na Biashara kwenye Uwanja wa Mkapa, mastaa wake wako kwenye mudi nzuri baada ya kupokea ujumbe wa kuvutia kutoka kwa mmoja wa wadhamini wa klabu hiyo, Ghalib Said Mohamed ‘GSM’.

GSM ambaye hivi karibuni alijiondoa kwenye udhamini wa ligi, amefanya kikao na mastaa wa Yanga Jumapili iliyopita kilichoambatana na bata flani hivi ndani ya jumba lake la kifahari lililopo hatua 35 kutokana ilipo kambi ya timu hiyo eneo la Kigamboni, Jijini Dar es Salaam.

Katika kikao hicho, licha ya GSM kuhudhuria na hakuongea kitu, lakini aliwatumia wasaidizi kuwafikishia ujumbe wachezaji na makocha wote mzigo wa posho umeongezeka na hataki tena kusikia matokeo yasiyofurahisha katika mechi zao kuanzia ya jana usiku.

Yanga wameambiwa kama shida yao ni fedha basi wapigane katika kila dakika 90 zilizo mbele yao na kila ushindi Milioni 25 itakuwa mezani kwa ajili yao.


 
Posho hizo ni ongezeko lingine la asilimia 25 kutoka kwa tajiri huyo na msimu huu walianza na posho za Sh20 Milioni kwa ushindi wa mechi moja ambazo sasa zimepanda zaidi.

Mbali na hapo msimu uliopita wachezaji wa Yanga walikuwa wanachukua kiasi cha Sh15 Milioni kwa ushindi wa mchezo na msimu huu zikapanda kwa asilimia 25 wakivuna Sh20 Milioni kwa kila mechi walizoshinda katika kuongoza kwao ligi na kufikia hatua ya robo fainali ya Kombe la Azam Shirikisho.

Hatua hiyo imeamsha mzuka mkubwa kwa wachezaji wa timu hiyo ambao wameahidi kikaoni kurudi na nguvu kuanzia mechi ya jana kisha ule wa Mtibwa Sugar wa kufunga mzunguko wa kwanza wa ligi.


“Tumewaambia vijana kazi ni kwao kama kweli wanataka fedha hizi sio tatizo tunachotaka ni kuona timu inashinda na ndio maana unaona GSM wamekuwa wakiboresha kila kitu kuhusu mahitaji yao ili akili zao zijikite katika kutafuta ushindi,” alisema bosi huyo mkubwa ndani ya Yanga na kamati ya mashindano.

Mzuka huo ukaleta vurugu mpya ndani ya kikosi hicho na kocha wao Nesreddine Nabi amegeuka mbogo akipiga mkwara mwenye ubora wa kuleta matokeo ndio atavaa jezi kuipigania timu hiyo.

Nabi kuanzia mchezo wa jana alitarajiwa kupangua kwa kiasi kikubwa kikosi chake akitaka kuona kila mtu aliye katika ubora anapata nafasi huku akivunja ukimya hakuna mchezaji mwenye umiliki wa nafasi ndani ya kikosi chake.

Mwanaspoti linafahamu sura mpya kadhaa zilikuwa zinatarajiwa kuanza akiwemo staa wao mpya wa TP Mazembe, Chico Ushindi ambaye alianza katika mechi ya kwanza ya mashindano tangu asajiliwe dirisha dogo.


 
Ushindi alichukua nafasi ya Jesus Moloko ambaye alipumzishwa huku sura zingine mpya zikiwa beki Paul Godfrey ‘Boxer’akianza kama beki wa kulia ambapo anaziba nafasi ya Djuma Shaban na Dockson Job ambao wamesimamishwa.

Hata hivyo, Djuma amemaliza adhabu yake ya kusimamishwa mechi tatu katika mchezo wa jana dhidi ya Biashara akirejea kazini kuvaana na Mtibwa Sugar.

Alipoulizwa kuhusu motisha hizo, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Yanga, Senzo Mbatha alisema lengo ni kuwaongezea morali ili waweze kupambana vya kutosha kwenye mechi zao.

Alisema kwa upande wake hawezi kuzungumzia sana mambo ya ndani kwani ni siri ya klabu na akadokeza; “Nipo nyumbani (Sauzi) nitarudi kesho huko, posho zipo katika kila mechi na wachezaji wanalipwa kwa wakati husika bila kuchelewa na hii ni kuzidi kuwapa motisha, hilo la kuongezeka sitaki kulizungumzia sana, lakini ukweli posho zipo na nzuri sana kwa wachezaji wetu.”


Yanga imepania kufanya makubwa msimu huu kwa kurejesha makombe waliyoyapoteza kwenye miaka ya hivikaribuni.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad