Yanga Mechi nne tu Freshi...Ndoo Wanaibeba



KIKOSI cha Yanga kimerejea jijini Dar es Salaam jana kutoka Morogoro baada ya kumaliza mechi za duru la kwanza ya Ligi Kuu Bara kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mtibwa Sugar, tayari kwa michezo ya duru la lala salama.

Yanga ilipata ushindi huo kwenye mechi iliyopigwa Uwanja wa Manungu, huku kocha wake akisema kazi haijaisha, lakini ikibainika kikosi hicho kitacheza mechi nne nje ya Dar es Salaam na ikitoboa hapo tu freshi kwao katika mbio za ubingwa.

Katika mechi 15 za duru la kwanza, Yanga imecheza michezo tisa ugenini na sita nyumbani na ikashinda 12 na kutoka sare tatu na kukusanya jumla ya pointi 39 na mabao 25 na kufungwa manne tu.

Katika mechi zao za duru la pili, Yanga itacheza mechi sita ugenini na tisa za nyumbani, lakini usichokijua ni kwamba katika mechi hizo sita za ugenini ni nne tu ndizo itasafiri kwenda mkoani na zilizosalia itakuwa jijini Dar es salaam.


Mechi nne za mkoani ambazo ikitoboa kama ilivyofanya kwenye duru la kwanza litaiweka Yanga katika nafasi nzuri ya kubeba ubingwa na mechi hizo ni dhidi ya Geita Gold watakaoanza nao baada ya kumalizana na Kagera Sugar keshokutwa.

Mechi nyingine ni dhidi ya Biashara United, Mbeya City na Dodoma Jiji, huku mechi nyingine dhidi ya Azam na Ruvu Shooting zitachezwa Dar es Salaam, labda tu kama timu hizo zitaamua kuzipeleka mikoani kama ilivyofanya KMC katika duru la kwanza walipoipeleka Yanga mjini Songea, mkoani Ruvuma.

Mechi hizo mbili za Ruvu na Azam zikiungana na nyingine tisa za nyumbani za Yanga dhidi ya Simba, Namungo, Kagera Sugar, Polisi Tanzania, Coastal Union, Mbeya Kwanza, Tanzania Prisons, Mtibwa Sugar na KMC zitaifanya Yanga icheze mechi 11 za duru la pili, huku ikibebwa na rekodi yao ya duru la kwanza.


Katika mechi sita za nyumbani za awali, Yanga ilishinda tano na kutoka sare moja, ikiwa na maana ilipoteza pointi mbili, wakati zile za ugenini ilishinda saba na kutoka sare mbili ikiwa na maana ilipoteza pointi nne hadi sasa.

Hata hivyo mechi za nyumbani zinazoonekana huenda ikaisumbua Yanga kulingana na rekodi dhidi ya wapinzani wao ni dhidi ya watetezi, Simba, Azam, Namungo, Polisi Tanzania na Tanzania Prisons, kwani zimekuwa zikisumbua.

Katika mechi za duru la kwanza timu hizo zote ukiondoa Simba na Namungo zilizotoka sare, nyingine zilichezea vichapo toka kwa vinara hao.

MSIKIE NABI

Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi amefunguka kuwa, licha ya kumaliza duru la kwanza kibabe, lakini bado kazi haijaisha kwa timu hiyo klwa vile safar8i ya ubingwa inaanzia kwenye duru la pili ikianza kuvaana na Kagera.


Akizungumza na Mwanaspoti Nabi alisema kikosi chake kimetumia mechi 15 kuthibitisha ubora wao msimu huu, lakini sasa wanakwenda kuianza safari ngumu ya kuhakikisha wanachukua mataji.

Nabi alisema duru la pili litakuwa gumu zaidi na kwa sasa wanaenda kupanga mikakati maalumu ya kila mchezo ili kuhakikisha hawasangushi pointi zozote.

“Nafikiri sisi ndio timu iliyocheza kwa ubora zaidi hizi mechi zote 15 tumefanya vizuri nyumbani na ugenini ukiweka mbali hizi sare tatu tulizopapa,”alisema Nabi na kuongeza;

“Duru la pili haliwezi kuwa rahisi nimewaambia wachezaji wangu tutakutana na ugumu mara mbili ya ule wa duru la kwanza.


“Hakuna timu itakayokuja kwetu ikubali kupoteza kirahisi.”

Nabi alisema timu imekuwa ikishinda kwa ubora walionao japo haikuwa rahisi kwani kila timu ilikuwa ikipania na kwamba anafurahi kuona sasa ubora wa wachezaji wake umekuwa ukiongezeka.

Juu ya mechi tisa za nyumbani, Nabi alisema bado haiwapi nafasi ya kuchukulia wepesi, akikumbushia sare ya kushtukiza ya nyumbani ni dhidi ya Mbeya City.

Naye Mkurugenzi wa Mashindano wa Yanga, Thabit Kandoro akitamba msimu huu ni wa Yanga kutokana na namna kikosi chao kinavyopambana kila merchi.

Kandoro alisema, kumaliza mechi 15 bila ya kupoteza ni juhudi za wachezaji na benchi la ufundi kufikia malengo waliyojiwekea.


“Yanga tuna kiu na ubingwa na nia tunayo ndio maana kila mchezo wachezaji wetu wanapambana ili kuvuna pointi tatu popote walipo.”

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad