Yanga: Sisi Sio Wao walioshindwa kuutafuna mfupa wa Mbeya City



YANGA wamepania kuwapoka Simba ubingwa wa Ligi Kuu Bara, ni baada ya kuwatumia tiketi za ndege mastaa wao watatu ili wauwahi mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Mbeya City.

Yanga pia wametoa kejeri wakisema wao sio kama Simba walioshindwa kuutafuna mfupa wa Mbeya City, na kwamba wanakwenda kuwachapa Mbeya City kwa Mkapa ili kujitofautisha na Msimbazi.

Wachezaji wao waliowatumia tiketi hizo za ndege ni kipa namba moja raia wa Mali, Djigui Diarra aliyepo katika kikosi cha timu ya taifa kilichokuwa kinashiriki Afcon 2021.

Mastaa wengine wawili ni Yannick Bangala na Shaaban Djuma wote waliitwa katika timu ya taifa ya DR Congo iliyocheza mchezo wake wa kirafiki wa kujiandaa na kufuzu Kombe la Dunia.


Yanga, leo Jumamosi saa 1:00 usiku, itajitupa kwenye Uwanja wa Mkapa kuvaana na Mbeya City ambao hivi karibuni wametoka kuwafunga Simba bao 1-0 nyumbani kwao kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Akizungumza na Championi Ijumaa, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Yanga, Hassani Bumbuli alisema kuwa nyota hao wote hadi kufikia Alhamisi usiku wote walikuwa wameripoti kambini Kijiji cha Avic Town, Kigamboni nje ya Jiji la Dar es Salaam tayari kwa maandalizi ya mchezo huo.

Bumbuli alisema kuwa katika mchezo huo, kocha mkuu wa timu hiyo, Nasreddine Nabi, amepanga kupanga full kikosi chake cha kwanza akiwemo Diarra, Bangala, Khalid Aucho na Said Ntibanzokiza ‘Saido’ ambao walikosekana katika mchezo uliopita wa hatua ya 32 bora ya Kombe la FA.


Aliongeza kuwa, mchezo huo wanauchukulia umuhimu mkubwa wa kushinda ili waendelee na rekodi nzuri ya matokeo mazuri ambayo tangu kuanza kwa msimu, hawajapoteza mchezo wowote.

“Tunafahamu umuhimu mkubwa wa mchezo wetu unaofuatia wa ligi ambao tutacheza Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Mkapa dhidi ya Mbeya City.

“Katika kuchukulia umuhimu wa mchezo huo, haraka uongozi umewatumia tiketi za ndege wachezaji wetu watatu waliokuwepo katika majukumu ya timu zao za taifa kwa ajili ya kuwahi mchezo huo.

“Diarra aliyetakiwa kutua nchini tangu Jumatatu, yeye ataungana na wenzake akina Bangala na Djuma tayari kwa ajili ya kujiunga na kambi ya pamoja na wenzake.

“Katika mchezo huo kocha Nabi amepanga kuwatumia wachezaji wote wa kikosi cha kwanza ambao walikosekana mchezo wa Kombe la FA dhidi ya Mbao FC, atakayekosekana ni Djuma pekee anayetumikia adhabu ya kufungiwa michezo mitatu,” alisema Bumbuli.

Bumbuli aliongeza kwa kutupa kijembe kwa Simba, akisema Mbeya City wanawaonea Simba pekee lakini siyo Yanga hii.

“Mchezo wetu ujao wa ligi dhidi ya Mbeya City ni mgumu, lakini hiyo haitufanyi tuwaogope kwani hao wanaogopwa na Simba, lakini siyo Yanga. Kikubwa tunajivunia ubora wa kikosi chetu cha msimu huu ambacho kina malengo ya kutwaa ubingwa wa ligi na hilo linawezekana kwetu,” alisema Bumbuli
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad