Tetesi za Baadhi ya wachezaji wa Young Africans kuwa mbioni kuondoka klabuni hapo mwishoni mwa msimu huu, zimezimwa na Uongozi wa ‘WANANCHI’ kwa kutoa kauli ya matumaini kwa Wanachama na Mashabiki.
Wanaotajwa kuwa mbioni kuikacha Young Africans kwa kisingizo cha mikataba kumalizika mwishoni mwa msimu huu ni Nahodha na Beki wa Kati Bakari Nondo Mwamnyeto na Beki wa Pembeni Shomari Kibwana.
Simba SC inatajwa kuwa kwenye mpango wa kuzinasa saini za wachezaji hao, huku ikielezwa tayari Uongozi wa klabu hiyo ya Msimbazi umejipanga kuzungumza na mameneja wao.
Uongozi wa Young Africans umesema kuwa wanaotajwa kujipanga kuwasajili Mwamnyeto na Kibwana wanajisumbua na badala yake mastaa hao wataendelea kukipiga Jangwani.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya Uongozi wa klabu hiyo kongwe katika ukanda wa Afrika Masharini na Kati zinaeleza kuwa, wachezaji hao wameshamaliza mazungumzo ya awali kwa ajili ya kuongeza mikataba kuendelea kukipiga klabuni hapo.
Taarifa hizo zimeongeza kuwa, kabla ya kuanza mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara, baadhi ya wachezaji hao watakuwa wamesaini mkataba baada ya kukamilishiwa mahitaji yao muhimu ikiwemo mshahara.
Wengine wanaomaliza mikataba yao YoungA fricans mwishoni mwa msimu huu ni Dickson Job, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ (mabeki), Saidi Ntibazonkiza ‘Saido’ , Yacouba Songne na Deus Kaseke (Viungo Washambuliaji).