Zitto: Kama siyo ‘kelele’ za Chadema Mbowe angetoka



Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe akijibu maswali ya wahariri wa habari baada ya kumaliza kutangaza wasemaji wa Kisekte (Baraza Kivuli la Mawaziri) walioteuliwa na kiongozi wa Chama hicho jijini Dar es Salaam.
Dar es Salaam. Kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amesema kama siyo kusakamwa na makada wa Chadema, baada ya kutoa ombi la kuachiliwa kwa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kwa Rais Samia Suluhu Hassan, angekuwa ameshaachiwa.

Mbowe alikamatwa Julai 2021 na kuunganishwa na washitakiwa wengine watatu ambao kwa pamoja wanashitakiwa kwa makosa ya ugaidi.

Desemba 15, 2021 Zitto akizungumza katika mkutano wa vyama vya siasa ulioandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa jijini Dodoma, alimwomba Rais Samia kuwezesha kuachiwa kwa Mbowe.

Hata hivyo, kauli hiyo iliibua hasira kwa baadhi ya makada wa Chadema, wakisema kuwa kitendo hicho ni sawa na kumwombea msamaha Mbowe kwa kosa ambalo hajafanya.


 
Leo tena, Februari 06, akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam, Zitto amesisitiza kuwa, alikuwa sahihi kumwomba Rais Samia.

“Naamini kupitia mkutano uliofanyika Dodoma kama kusingekuwa na kelele zile na kuwa pamoja naamini pengine Mbowe angekuwa nje kwa sasa i believe that,” amesema Zitto.

Zitto aliendelea kusema kuwa kati ya mambo yanayomuumiza kichwa kwa sasa ni kuona akiwa bado rumande akiendelea na kesi inayomkabili.

 “Mimi Mbowe ni amenilea. Ninavyomuona yupo jela simuoni kama kiongozi wa Chadema yupo jela ‘I see my brother. Yupo jela napambana kuona anatoka jela as my brother lakini si Mwenyekiti wa Chadema.

“Nimekwenda jela kuzungumza naye kumuambia hiki naenda kukifanya alinijibu mdogo wangu kafanye. Wao wanamuona mwenyekiti wao yupo jela, mimi namuona kaka yangu ni vitu viwili tofauti najisikia vibaya kila siku kumuona anaenda Mahakamani na kurudi,” amesema Zitto.

Katika mkutano huo, Zitto alitangaza Baraza la wasemaji wa kisekta la chama hicho.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad