Acha vita hii': Arnold Schwarzenegger amwambia Putin



Los Angeles, Marekani (AFP). Nyota wa filamu ya "Terminator", Arnold Schwarzenegger amemtaka Vladimir Putin kuacha vita "isiyo na maana" nchini Ukraine na kuwasifu wananchi wa Russia kwa kuandamana kupinga mzozo huo, akisema ni mashujaa wapya.

"Ukraine haikuanzisha vita hii," alisema gavana wa zamani wa California katika ujumbe wenye hisia kwa wananchi na wanajeshi wa Russia alioutuma katika akaunti yake ya Twitter na mitandao mingine.

"Nazungumza nanyi leo (Alhamisi) kwa sababu kuna mambo yanaendelea duniani na ambayo mnafichwa, vitu vibaya ambavyo mnatakiwa mvijue," amesema katika video hiyo ya dakika 11 ambayo ilikuwa na maandishi ya lugha ya Kirussia.

Bingwa huyo wa zamani wa kutunisha misuli na mzaliwa wa Austria na ambaye filamu yake ya "Red Heat" ilikuwa ya kwanza ya Kimarekani kuonyeshwa katika bustani ya Red Square jijini Moscow, alizungumzia mapenzi yake kwa wananchi wa Russia na kukutana na mtu aliyekuwa anamhusudu kwa kunyanyua vitu vizito, Yuri Vlasov wa Russia wakati akiwa na miaka 14.


 
"Uimara na moyo wa watu wa Russia umekuwa ukinivutia," alisema. "Ndio maana natumaini mtaniruhusu kuwaambia ukweli kuhusu vita vya Ukraine. Najua kuwa serikali yenu imewaambia kuwa hii ni vita ya kuuondoa Unazi nchini Ukraine. Hiyo si kweli. Watu wa Kremlin walioko madarakani walianzisha vita hii. Hii si vita ya wananchi wa Russia."

Schwarzenegger alisema "dunia imepingana na Russia kutokana na vitendo vyake nchini Ukraine -- majengo yote ya jiji yameangushwa na mabomu ya Russia, ikiwemo hospitali ya watoto na wodi ya wajawazito.

"Kutokana na ukatili wake, Russia sasa imetengwa kutoka jumuiya ya mataifa," alisema.


Katika ombi lake kwa wanajeshi wa Russia, Schwarzenegger anakumbuka majeraha aliyopata baba yake wakati akipigania majeshi ya Nazi wakati wa Vita Kuu vya Pili vya Dunia.

"Alivunjika kimwili na kiakili na kuisha maisha yake yote yaliyosalia kwa uchungu," alisema. "Kwa wanajeshi wa Russia wanaosikiliza video hii... sitaki muumie kama baba yangu.

"Hii si vita ya kuilinda Russia ambayo mababu zenu walipigana. Hii ni vita isiyo halali. Maisha yenu, viungo vyenu, hali  yenu ya baadaye imetolewa mhanga katika vita isiyo na maana inayolaaniwa na dunia nzima."

Akimwambia Putin moja kwa moja, Schwarzenegger amesema: "Ulianzisha vita hii. Unaongoza vita hii. Unaweza kuisimamisha."

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad