Aden Rage motoni baada ya kukejeli 'Ligi Kuu'



Mwenyekiti wa zamani wa Simba, Ismail Aden Rage amejikuta akishambuliwa vikali na mmoja wa wanachama wa klabu hiyo, Festo Sanga baada ya kuiponda michuano ya ubingwa wa soka wa Tanzania.

Katika moja ya video zilizotoka baada ya Simba kuishinda RS Berkane ya Morocco kwa bao 1-0 katika mechi ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho, Rage anahojiwa na waandishi kuhusu mchezo huo.

"Kwa hiyo leo Simba wanaongoza kwa kuwa na pointi saba. Kwa hiyo tumebakiza mechi moja tu, twende halafu tuwaachie hili kombe lenu la mbuzi mshindane wenyewe. Sisi huko kwenye kupanda ndege," anasema Rage katika video hiyo.

"Ukishinda na kuwa bingwa wa Kombe la Shirikisho, huna sababu ya kucheza haya mashindano ya kombe la mbuzi. Kule kuna dola milioni 3.5, huku kuna shilingi laki moja. Sasa wapi unapenda rafiki yangu."


 
Maneno hayo yalimfanya Sanga, ambaye ni mbunge wa Makete aingie mtandaoni kumjibu katibu huyo wa zamani wa Chama cha Soka (FAT).

“Ligi Kuu Tanzania Bara, SIO LIgi ya Mbuzi. Hii ndio Ligi iliyoifanya Simba ikacheza CCL (Ligi ya Mabingwa) na Shirikisho Africa," ameandika Sanga katika akaunti yake ya Instagram.

"Hii ndio Ligi (ambayo) serikali na sekta binafsi inawekeza fedha zake na kuajiri maelfu ya Watanzania. Hii ndio Ligi ilikufanya RAGE uitwe RAGE nchi hii. TUJIZUIE..., PERIOD.”


Ni kawaida kwa mashabiki wa klabu za Yanga na Simba kutaniana kwa kuitana au kujisifia kwa maneno kama "wa matopeni" au "wa kimataifa" au "wa Kombe la Mbuzi" kumaanisha michuano ya mitaani, kila moja ya timu hizo inapokuwa inashiriki mashindano ya kimataifa.

Lakini ni nadra kwa kauli hizo kutolewa na viongozi, isipokuwa katika siku za karibuni maofisa habari wamefikia kiwango cha kutumia maneno kama hayo kukashifiana mitandaoni au katika mikutano na waandishi wa habari.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad