Adhabu Tatu zamsubiri Kamanda Wankyo



Dar es Salaam. Mdomo uliponza kichwa, hivi ndivyo inaweza kuelezewa kwa kilichomkuta aliyekuwa Kamanda wa Polisi mkoani Kagera, Wankyo Nyigesa baada ya kutenguliwa kwenye nafasi hiyo aliyodumu kwa siku 56.

Wankyo alianza kutikisa kwenye vyombo vya habari, hususan mitandao ya kijamii siku chache zilizopita kufuatia kauli yake kuwa anatamani wadhifa wa juu zaidi ndani ya jeshi hilo ambao ni ukuu wa Jeshi la Polisi (IGP), jambo ambalo limetafsiriwa kuwa ni utovu wa nidhamu kulingana na miongozo ya jeshi hilo.

Juzi, Jeshi la Polisi kupitia msemaji wake, David Misime lilitoa taarifa kwa vyombo vya habari ya mabadiliko ambayo yamemtoa Wankyo katika wadhifa wake wa U-RPC na kurudishwa makao makuu ya jeshi Dodoma, huku nafasi yake ikijazwa na aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Kamishna Msaidizi wa Polisi, William Mwapagale.

Wankyo amekumbana na uhamisho huo ikiwa ni siku 56 tangu ahamishiwe mkoani Kagera akitokea Mkoa wa Pwani ambako alifanya kazi kwa miaka miwili.


Taarifa hiyo ya Misime iliweka wazi kuwa uhamisho huo umefanyika kupisha uchunguzi dhidi ya kauli aliyotoa Wankyo na kuwa suala hilo limeanza kufanyiwa kazi na matokeo ya uchunguzi yatafikishwa kwenye mamlaka husika za kinidhamu kwa hatua zaidi.

Kufuatia hatua hiyo, vyanzo mbalimbali ndani ya Jeshi la Polisi vimeeleza kuwa adhabu tatu zinaweza kumkumba kamanda huyo.

Wankyo alipotafutwa na Mwananchi kwa njia ya simu ili azungumzie tukio hilo, simu yake iliita bila kupokewa.


Chanzo chake

Sakata hilo lilianzia katika hafla ya kumuaga iliyofanyika Kibaha mkoani Pwani, ambako Wankyo alitamka hadharani matamanio yake ya kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi na kuahidi endapo atateuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan, atafanya kazi hiyo kwa ufanisi mkubwa.

“Nilikuwa najiandaa kuwa DCI lakini nafasi ya DCI ikachukuliwa, nikajiandaa kuwa Kamishna Polisi wa Zanzibar wakachukua, sasa hivi najiandaa kuwa IGP na ninaamini Rais Samia maombi yangu anayasikia, siku moja tafadhali niteua Wankyo kuwa IGP.

“Mimi naamini nitafanya makubwa, huwa ninaomba sana Mama, siku moja aniote tu halafu anitamke tu niwe IGP.Mimi nitamuomba nifanye miaka mitatu halafu nimwambie mama nakukabidhi naondoka, unaonaje hapo?” alisema Wankyo.

Aliendelea kusema, “Najua IGP aliyepo hajafanya makosa, anafanya mazuri lakini mimi nitafanya mazuri zaidi, binadamu lazima uote ndoto kubwa, siwezi kuendelea kuota kubaki kamanda, nataka niote nafasi hizo kubwa ili nifanye makubwa kwa faida ya Watanzania wengi kuliko ninavyofanya sasa kwa mwaka mmoja.


“Kama mheshimiwa Rais ataomba kwa Mungu akamuonyesha mimi, hatakuwa amekosea, atakuwa amepata mtu sahihi kwa wakati sahihi,” alisema.

Kulingana na mwongozo wa Jeshi la Polisi, Wankyo ni mteule wa Rais kulingana na cheo alichonacho, hivyo hatima yake ipo mikononi mwa Rais Samia, hata hivyo kwa mujibu wa sheria na taratibu za kijeshi, ofisa wa cheo chake anapofanya kosa la aina hiyo na likathibitika, inaelezwa kuwa IGP anaweza kupendekeza kwa Rais avuliwe cheo au astaafishwe kwa manufaa ya umma au akapewa onyo.

Septemba 24, 2019 akiwa katika ufunguzi wa kikao kazi cha maofisa waandamizi wa polisi kilichofanyika jijini Dar es Salaam, IGP Sirro alisema tatizo linalolisumbua jeshi hilo ni unafiki na alisisitiza kuwa mwenye wadhifa kama wake yupo mmoja tu.

“Tatizo linalotusumbua sisi Jeshi la Polisi pia ni unafiki. There is no way (hakuna njia) tukawa na IGP zaidi ya mmoja, mimi sikujichagua. Natamani kumaliza nafasi yangu Jeshi la Polisi likiwa na heshima yake. Jeshi hili ikiharibika tumeharibikiwa wote na mimi siwezi kumuwekea mtu kinyongo, mie si wa aina hiyo, kwa hiyo niwaombe ushirikiano,” alisema IGP Sirro.


Sirro aliteuliwa kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi Mei 28, 2017 na Rais John Magufuli, akichukua nafasi iliyoachwa na Ernest Mangu, aliyeteuliwa na Magufuli kwenda kuwa balozi, na amekaa kwenye wadhifa huo kwa miaka mitano huku kukiwa na tetesi kuwa anakaribia kustaafu.

Limekaaje kijeshi

Baadhi ya maofisa wa polisi walioko kazini na waliostaafu waliozungumza na Mwananchi kwa sharti la kutotajwa majina yao gazetini, walilieleza kuwa tangu video ya Wankyo ilipoanza kusambaa, waliona ina matatizo mawili, moja la kudharau mamlaka juu yake kwa maana ya IGP na la kudharau cheo cha Rais.

“Mamlaka ya uteuzi wa RPC ni ya IGP, lakini anayetia saini kuidhinisha ni Rais. Sasa kama labda court martial (mahakama ya kijeshi) itaona ana makosa ndio watapendekeza adhabu anayoweza kuitoa Rais kwa mhusika,” alisema ofisa mmoja.

Mwingine alisema ili kulithibitisha hilo, ni lazima iundwe timu ya maofisa waandamizi walio juu yake ambao watachunguza kosa hilo na kulitolea mapendekezo ya kipi kifanyike. “Na mara nyingi timu hii hufanya kazi kama mahakama kabisa na kama watabaini kosa ni kubwa, wataweza kupendekeza ashushwe cheo,” alisema.

Ofisa mwingine ambaye amestaafu akiwa na cheo cha Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP), ambaye naye hakutaka kutajwa jina, alisema kuna maneno ambayo RPC huyo aliyazungumza yalimaanisha kuwa IGP aliyepo hatoshi.


“Ukimsikiliza anaomba ateuliwe kuwa IGP halafu anasema atafanya mambo makubwa zaidi. Tafsiri yangu mimi ni kwamba alikuwa anamsema indirect (sio moja kwa moja) IGP ambaye ni bosi wake kuwa hafanyi vizuri,” alidai.

Kwa mujibu wa ofisa mwingine ambaye yuko kazini, endapo Wankyo atabainika kutenda kosa hilo kwa kudhamiria, adhabu yake inaweza kuwa kunyang’anywa cheo au kustaafishwa kwa manufaa ya umma.


Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad