Mahakama ya wilaya ya Babati Mkoani Manyara imemhukumu Gusurugusta Ginanai(35) mkazi wa Serengeti kwenda jela miaka 19 kwa kosa la wizi wa fedha mtandaoni.
Akisoma hati ya mashtaka mwendesha mashtaka wa serikali Grace Mgaya alisema mshtakiwa Julai 23 mwaka 2020 hadi Agost 18 mwaka 2020 akiwa Kijiji cha Orbesh kilichopo wilaya ya Babati aliiba sh. Milioni mbili kutoka Benki ya CRDB kwenye akaunt namba 0152297915900 ya Martin Pamoki ambaye alimuomba kumfanyia muamala kupitia Simbanking kwa simu yake ya mkononi.
Mgaya alidai watu hao walikutana Kijiji cha Orbesh ambapo mlalamikaji alikuwa anatibiwa macho kwa kutumia dawa za asili ndipo alimuomba amsaidie kuhamisha fedha.
Aidha alisema mshtakiwa siku iliyofuata alimuomba simu Pamoki ili aweze kuwapigia ndugu zake alipopewa simu ndipo alihamisha fedha nyingine kwenda akaunt zake tofauti.
Alisema mshtakiwa kwa kuwa alikuwa na namba za siri alihamisha sh. Mil. 31.250 na kutokomea kusikojulikana.
Baada ya Pamoki kubaini ameibiwa aliripoti kituo cha polisi Babati ndipo polisi walianza msako na kumnasa akiwa Mkoani Katavi amejificha.
Akisoma hukumu hiyo jana Hakimu mkazi Mfawidhi wa mahakama ya wilaya ya Babati Victor Kimario alisema baada ya kujiridhisha pasipo shaka mshtakiwa amemtia hatia na kumtaka kutumikia kifungo cha miaka 19 jela.
Kimario alisema mshtakiwa alikutwa na makosa 19 ambapo kila kosa amemhukumu kwenda jela mwaka mmoja na jumla yake kutumikia miaka 19.
Hakimu huyo alisema mshtakiwa alitenda kosa la wizi kinyume na sheria ya kanuni ya adhabu namba 258(1) na 265 cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2019.
Alipopewa nafasi ya kujitetea mshtakiwa alisema anaomba aachiwe huru kwa kuwa ana familia kubwa inamtegemea.