Mwanaume mmoja ambaye ni raia wa Jamhuri ya kidemokrasia ya congo aliyetambulika kwa jina la Luwizo ameingia kwenye rekodi ya mfalme Solomoni wa vitabu vya dini baada ya kuoa wanawake 3 kwa pamoja ambao ni pacha.
Luwizo alifanya harusi na pacha watatu wanaofanana katika harusi ya kufana lakini ni mwanamume mwenye wake wengi kutoka Kalehe, Kivu Kusini, DR Congo.
Mapacha hao watatu Natasha, Natalie, na Nadege katika sherehe ya harusi yao walipendeza kwa kuvalia gauni nyeupe zijulikanazo kama shela.
Natasha, Natalie, na Nadege katika sherehe ya harusi yao
Katika mahojiano na AfriMax, Luwizo alifichua kwamba mwanzo Natalie ndiye alikuwa ameteka moyo wake baada yao kukutana kwenye mtandao wa kijamii lakini kila Luwizo alipokuwa akimtembelea Natalie nyumbani kwake, na kumkosa, alikuwa akikaribishwa na mmoja wa pacha hao ambao alishindwa kuwatofautisha.
Siku zilipoendelea kusogea pacha wote watatu walichanganywa na penzi lake na Luwizo alisema alishtuka kukuta warembo hao wakimwambia wanataka awaoe wote pale alipokwenda kutaka idhini ya Natalie ili amuoe.
“Mwanzoni tulipomwambia kwamba anatakiwa kutuoa sote alishtuka, lakini kwa sababu tayari alikuwa ametupenda sote, hakuna kitu ambacho kiliweza kuzuia mipango yetu kwani pia tulikuwa tunampenda, watu wanaona kuwa haiwezekani kwa wanawake watatu kugawana mume mmoja, lakini kwetu, kugawana kila kitu imekuwa maisha yetu tangu utotoni,” Natalie, mmoja wa mapacha hao watatu alisema.
Akizungumzia tukio hilo Luwizo alisema, “Karibia nizimie. Nikawauliza kati yenu nyote, Natalie ni nani? Wakaniambia nimekutana nao siku tofauti tofauti nilizomtembelea. Nilichanganyikiwa kwani nilikuwa na mpango wa kumuoa Natalie lakini kilichonichanganya ni kwamba nisingeweza kuoa mmoja wao na niwaache wale wawili.”
Luwizo akiwa na wakeze Natasha, Natalie, na Nadege
“Nililazimika kuwaoa wote kwa sababu ni mapacha watatu. Haukuwa uamuzi rahisi kwa sababu hadi sasa, wazazi wangu hawaelewi ninachofanya.” Aliongeza.
Luwizo amekuwa katika ndoa na pacha hao watatu kwa mwezi mmoja sasa ambapo alibadilishana viapo vya ndoa na pacha hao katika hafla ya faragha iliyohudhuriwa na marafiki wa karibu na familia ingawa wazazi wake hawakuhudhuria harusi hiyo.
“Lazima upoteze kitu ili upate kingine. Isitoshe, mtu ana matakwa yake na namna yake ya kufanya mambo. Kwa hiyo nina furaha kuwaoa hao mapacha watatu bila kujali wengine wanafikiria nini. Wazazi wangu walidharau uamuzi wangu ndiyo maana waliona wasihudhurie harusi yangu. Lakini ninachoweza kusema ni mapenzi hayana kikomo,” alisema.
Akizungumzia ndoa yao, Natalie ambaye ndie alifungua njia ya ndoa hiyo kwa kukutana na Luwizo, alisema, “tuna furaha sana. Ndoto yetu ilitimia. Tulifikiri tungetenganishwa na ndoa, lakini Mungu alisikia maombi.”
“Mwanzoni niliposikia anaoa mapacha watatu sikuelewa lakini baadaye nikaelewa inawezekana, ingawa wazazi wetu walimdharau, nitamuunga mkono kila wakati,” Dada yake Luwizo alisema.
Aliongeza kuwa amefurahishwa naye na ataunga mkono uamuzi wake kila wakati.