OFISA Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez amesema hakuna wasiwasi wowote licha ya kupoteza ugenini mabao 3-0 dhidi ya Asec kwani timu hiyo inakwenda kucheza robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu.
Barbara alisema wanafahamu kuna mashabiki wengi wa Simba walikuwa na morali ya juu wakiamini timu yao inakwenda kupata matokeo mazuri kwenye mechi dhidi ya Asec Mimosas na kufuzu hatua inayofuata.
Kiongozi huyo alikiri kwamba msimu huu hajawahi kuona wachezaji wakiwa na morali ya hali ya juu kama ilivyokuwa kwenye mchezo wa juzi.
“Unajua tangu tulivyofika hapa Benin wachezaji, benchi la ufundi na viongozi tulioambana tulikuwa na morali ya hali ya juu na hamu kubwa ya kwenda kushinda mchezo huu na Mimosas ili kwenda kuweka rekodi klabu na nchi,” alisema Barbara na kuongeza;
“Kabla ya mechi kocha Pablo, alituambia mpango wake wa mechi na ulikuwa una faida ndani yake tukiamini tunakwenda kushinda na kuweka rekodi ya kufuzu robio fainali ugenini huku tukiwa na mechi moja mkononi,”
“Tulifanya kikao na wachezaji kabla ya mchezo yaani walikuwa na morali ya hali ya juu nieleze tu ukweli katika mechi zote za ugenini hawajawahi kuwa na hamu ya kushindana na hamasa kubwa kama ilivyokuwa kabla ya mchezo huu.
“Bahati mbaya wapinzani wetu wameweza kuwa bora na kutumia vyema mchezo wao wa nyumbani, Kama uongozi hilo kwetu limeisha na sasa nguvu na mipango tunaihamishia kwenye mchezo wa mwisho nyumbani dhidi ya USGN.
“Kabla ya kurudi nchini tutaongea na wachezaji kwani wengine wanakwenda katika majukumu ya timu za taifa ila tumekubaliana watambana mpaka jasho lao la mwisho kwenye mchezo wetu wa mwisho hatua ya makundi na kufuzu robo fainali ya mashindano haya.”
Barbara aliongeza wao viongozi watarudi na kuangalia namna gani wanatakiwa kuwapa nguvu benchi la ufundi na wachezaji ili kufanya kile wanachohitaji kwa wakati na kuhakikisha mchezo wa nyumbani wanaondoka na ushindi.
“Mashabiki wetu kazi yao ni moja kutuombea timu ifanye maandalizi vizuri, isitokee mchezaji yoyote akaumia na kushindwa kuwa sehemu ya mchezo siku ya mechi wajitokeze kwa wingi kulingana na nafasi ya kuingiza mashabiki tutakayopata na wote washangilie mwanzo mwisho tutafanikiwa kuweka rekodi nyingine ya kufuzu,” alisema Barbara.
Simba watacheza mechi ya mwisho hatua ya makundi dhidi ya USGN Aprili 3, katika Uwanja wa Benjamin Mkapa na wanahitaji ushindi bila kuangalia michezo ya timu nyingine ili kufikisha pointi kumi na kutinga robo fainali