Bilionea Abramovich Atorosha Boti Za Kifahari, Ndege Binafsi



BILIONEA wa Urusi, Roman Abramovich ambaye pia alikuwa mmiliki wa Klabu ya Chelsea ya Uingereza, ametorosha boti zake mbili za kifahari, Solaris na Eclipse zenye thamani ya dola za Kimarekani bilioni moja na ndege binafsi yenye thamani ya dola milioni 49 za Kimarekani akikwepa mali zake kutaifishwa.

 

Abramovich ni miongoni mwa mabilionea wa Urusi wanaondamwa na vikwazo vya kiuchumi kutoka mataifa mbalimbali yanayopinga uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, akitajwa kuwa na urafiki wa karibu na Rais Vladimir Putin wa Urusi.

 

Inaelezwa kwamba Abramovich ambaye alichukua uraia wa Israel mwaka 2018, baada ya kuanza kuwekewa vikwazo nchini Uingereza ikiwa ni pamoja na kuzuia mali zake zote, alikimbilia nchini Israel lakini serikali ya nchi hiyo nayo imeonekana kumuwekea ngumu, hali iliyomlazimu kuondoa mali zake kadhaa nchini humo na kurejea Moscow, Urusi.

 

Picha kadhaa zilizopigwa na Shirika la Habari la Reuters, zinamuonesha Abramovich akiwa katika Uwanja wa Ndege wa Ben Gurion jijini Tel Aviv, Israel akijiandaa kupanda ndege yake binafsi kuelekea Moscow huku ikielezwa kuwa boti zake zimetoroshwa kuelekea Istanbul, Uturuki na Moscow.

 

Hatua hiyo ya Abramovich, inakuja muda mfupi baada ya Umoja wa Ulaya (EU) nayo kutangaza kuanza kumuwekea vikwazo bilionea huyo na wenzake kuanzia Jumatatu ya Machi 15, 2022 ikiwa ni siku chache tangu Uingereza ilipotangaza vikwazo hivyo dhidi yake na mabilionea wenzake sita.

 

Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) kupitia kipindi chake cha panorama, Jumatatu ya wiki hii, ilirusha habari zinazodai kwamba Abramovich mwenye utajiri unaofikia dola za kimarekani bilioni 12, amekuwa akishirikiana na Rais Vladimir Putin katika biashara zenye harufu ya rushwa, ambazo zinatajwa kuwa ndiyo chanzo cha utajiri mkubwa anaoumiliki.

 

Taarifa katika kipindi hicho, ziliendelea kueleza kwamba BBC inao ushahidi wa jinsi Abramovich anavyonufaika na urafiki wake na Putin, ikiwemo kutumia mabilioni ya walipa kodi wa Urusi kujinufaisha.

 

Hata hivyo, muda mfupi baada ya kipindi hicho kurushwa, wanasheria wa Abramovich walijitokeza kupinga vikali madai hayo na kueleza kwamba mteja wao hajawahi kujihusisha kwa namna yoyote katika biashara ambazo ni kinyume cha sheria kwa lengo la kujinufaisha.

 

Katika vikwazo vilivyotangazwa na Uingereza wiki iliyopita, serikali ya nchi hiyo ilieleza kwamba Kampuni ya Evraz inayozalisha bidhaa za chuma ambayo inamilikiwa na Abramovich, ilishiriki kuisaidia Urusi kutengeneza vifaru vya kivita ambavyo vinatumika katika uvamizi nchini Ukraine.

 

Hofu ya mali za Abramovich, zikiwemo boti zake kudaiwa kutaka kutaifishwa, imetiwa nguvu na madai yaliyotolewa na wafanyakazi wa bandari ya Porto Montenegro Marina yakidai kwamba walipewa maelekezo kwamba boti za Abramovich zikitia nanga katika bandari hiyo, zizuiliwe kuondoka.

 

Taarifa zinaeleza kwamba Boti ya Kifahari ya Solaris, baada ya kuondoka nchini Israel, inaelekea katika Bahari ya Mediteranian, ikikwepa kupita katika pwani ya Ugiriki ambapo inatarajiwa kuwasili Uturuki wiki ijayo.

 

Boti nyingine ya Abramovich, Eclipse inaelezwa kwamba nayo imeonekana ikiondoka katika ukanda wa Caribbean, ikielekea nchini Libya kabla ya baadaye nayo kuelekea nchini Uturuki.

 

Miongoni mwa mali nyingine za mamilioni ya fedha zinazomilikiwa na bilionea huyo mkubwa, ni pamoja na jumba la kifahari la Kensington, jumba jingine la kifahari la penthouse, boti za kihafari, ndege binafsi, helikopta na magari ya bei mbaya na mali nyingine nyingi zilizopo sehemu mbalimbali duniani huku asilimia kadhaa ya mali hizo, zikiwa zimezuiwa nchini Uingereza.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad