Kihistoria Uturuki ilikuwa sehemu ya himaya kubwa ya Ottoman ambayo ilianza mnamo karne ya 13. Himaya hii ambayo ilianza kidogokidogo ilipanuka na kuwa kubwa zaidi wakati wa utawala wa Sultan Suleiman Khan au Suleiman The Magnificent kama ambavyo wazungu walimuita.
Unapokaa na kuangalia tamthilia hizi ujue unaangalia historia halisi ya himaya ya Ottoman iliyozaa Uturuki na hata Saudi Arabia ya sasa na Libya, Morocco na kadhalika. Na hii ndiyo inayonisukuma kutamani kina Ertugrul Beyi wangezaliwa Tanzania. Tamaa yangu inatokana na ukweli kwamba nchi yetu ina mikasa mingi zaidi ya ile iliyopo Uturuki ambayo kina Ertugrul wanatamba nayo.
Hii nchi ina makabila zaidi ya 120 na kabla ya Tanzania kuwa taifa kama lilipo leo, asilimia kubwa ya makabila yalijiendesha kama nchi kamili. Mkwawa na Wahehe wenzake pamoja na Wabena walikuwa katika nchi yao. Mazengo na Wagogo wenzake walikuwa kwenye nchi yao. Mirambo na Wanyamwezi wake walikuwa kwenye nchi yao. Hawa wote wana simulizi nzuri sana ambazo zingeweza kuwa tamthilia tamu na za kuvutia.
Vipi ikitokea JB akiigizia tamthilia ya ujio wa Wangoni nchini? Hivi ni nani aigize tamthilia ya vita vya Wangoni chini ya Chifu Mputa Gama na Songea Mbano dhidi ya Wahehe chini ya Munyigumba baba yake Mkwawa vilivyopiganwa pale Makambako?
Nani aigize tamthilia ya kipigo cha kwanza kabisa cha Wajerumani dhidi ya Mkwawa pale Lugalo Iringa? Kambi ya jeshi ya Lugalo - Dar es Salaam imerithi jina la eneo ambalo Mkwawa aliwashinda vita Wajerumani mwaka 1891. Hivi ndivyo vita vya kwanza kihistoria Wajerumani kushindwa na kamanda wao Zelewski kuuawa. Yaani Mjerumani alishindwa kwa mara ya kwanza katika ardhi yetu halafu tunachukulia poa tu.
Bahati mbaya hapa kwetu wamezaliwa kina Wema Sepetu, Kajala, JB, Idrisa Sultan na kadhalika ambao kazi zao nyingi ni za mapenzi tu, mapenzi yenyewe hawayawezi, yani ni vituko.
Tatizo kubwa la watayarishaji wa Filamu za kitanzania ni nini? Ufikiri, Elimu, Uvivu, Pesa, au??