Bosi Afichua Ishu ya Mayele Kusajiliwa Yanga, Haikuwa Rahisi



PENGINE kama viongozi wa Yanga wasingekuwa na uhakika wa kufanikisha usajili wa mshambuliaji Fiston Mayele raia wa DR Congo, basi leo hii mashabiki wa timu hiyo wasingekuwa wanatetema kwa furaha.

Mayele ambaye amejiunga na Yanga mwanzoni mwa msimu huu akitokea AS Vita ya DR Congo, amekuwa akiwapa raha mashabiki wa timu hiyo kutokana na umahiri wake wa kufunga mabao, huku staili yake ya kushangilia kwa kutetema ikiwa maarufu.

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili na Ufundi ya Yanga, Dominick Albinus, ameliambia Spoti Xtra kwamba, Wanayanga wanapoendelea kufurahia mafanikio ya timu yao msimu huu, wanapaswa kufahamu kwamba, haikuwa rahisi kumpata Mayele.

Albinus alisema: “Fiston Mayele tunakumbuka alikuja na timu yake ya taifa na alifunga bao ambalo ni la mtindo uleule akimfunga Manula (Aishi), msimu uliopita alikuwa mfungaji bora namba mbili kwenye Ligi ya DR Congo akiwa AS Vita akifunga mabao 14.


 
“Tulipomuona tukasema kuwa huyu anaweza kutusaidia sana kwa sababu ni mchezaji aliyekamilika.

“Tulianza kumfuatilia muda mrefu, kwa hiyo tukaongea na klabu yake, wakala wake na yeye mwenyewe. Klabu wakaturuhusu tukakaa mezani tukazungumza walikubali na tukamsajili.

“Katika usajili wake, tulikutana na changamoto kwani pia alikuwa anatakiwa na klabu nyingine kutoka Afrika Kusini na Misri, kwa hiyo tulichokifanya tuliwahi na tukamsainisha.


“Mwisho wa siku tukaanza kusikia kuwa hizo klabu tayari zilipeleka ofa zao lakini sisi tuliwahi, hicho ndicho kilichotufanya tukafanikiwa. Kama tungechelewa, tungemkosa.”

Mayele ndiye kinara wa mabao Ligi Kuu Bara msimu huu akiwa nayo kumi sawa na Reliants Lusajo wa Namungo.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad