Rais Samia Suluhu Hassan
MIAKA ya nyuma tukiwa watoto, shuleni tukijifunza Fizikia, walimu wetu walituelewesha nini maana ya chanya na hasi katika somo hilo na umuhimu wa pande hizo mbili. Anaandika Joseph Kulangwa, Dar es Salaam … (endelea).
Wakitwambia, hasi ikikutana na chanya huzaa nishati, ambao ni umeme na ndiyo sababu ya kuwapo betri, kwamba ukiunganisha pande hizo mbili cheche hutokea.
Sisi katika kufanya majaribio hayo, tukawa tunachukua betri za tochi au redio na kufunga waya wenye kitu kinaitwa glopu (bulb) ambayo iliwaka baada ya kukutanisha chanya na hasi.
Kwa umbile la betri hizo ambazo enzi hizo pia wazee waliziita mawe ya tochi au mawe ya redio, chanya ilikaa juu na hasi chini, hivyo tulipoweka glopu kwenye chanya ikiwa na waya kiunoni mwake huku sehemu nyingine ikiwa kwenye hasi, iliwaka.
Hapo ndipo tukagundua kuwa kumbe chanya na hasi lazima viwe pamoja, ili kuleta kitu tulichokitarajia, yaani bila chanya na hasi hakuna nishati ya umeme.
Lakini tulipoendelea kukua na kupanda madarasa, tukafikia ngazi ya kujifunza uzazi kwenye Biolojia au Elimu ya Viumbe, ambako tulifundishwa jinsi binadamu na wanyama wanavyozaliana.
Huko nako, tukakutana na yale yale ya chanya na hasi, kwamba mawili hayo yakikutana, ndipo viumbe huzaliana; kwamba chanya ni mwanamume na hasi ni mwanamke na wakutanapo kimwili, ndipo mimba hutungwa na mtoto kupatikana.
Bunge la Tanzania
Yote hayo yalilenga kutufundisha kuwa kumbe vipinganavyo ndivyo vizalishavyo kitu. Wengine wakafikia kutujulisha kuwa ndiyo sababu kuna mchana na usiku, kuna juu na chini, kuna kushoto na kulia, kuna Magharibi na Mashariki, Kusini na Kaskazini.
Yote hayo yalionesha pande mbili zinazozaa kitu kimoja muhimu sana, katika maisha na maendeleo ya viumbe hai wakiwamo binadamu. Hatimaye ndipo tukaingia kwenye siasa, tukakuta kuna tawala na pinzani.
Awali katika Tanzania wengine tulikuta nchi inaongozwa na chama kimoja cha siasa, lakini baadaye tukaambiwa upo umuhimu wa kuwa na vyama vingi vya siasa ili mambo yaweze kwenda.
Tuliojifunza Fizikia na Biolojia, tukakumbuka kuwa kumbe bila chanya na hasi hakuna kitu kitakwenda. Ilipoundwa Tume ya Jaji Francis Nyalali kwa saini ya Rais Ali Hassan Mwinyi, tukadhani ni maskhara.
Lakini baada ya Tume ile kuzunguka nchi nzima, kupata mawazo ya Watanznaia kama wanataka vyama vingi au wabaki na kimoja, majibu yakaja kuwa wengi walitaka kubaki na chama kimoja.
Tukaambiwa kuwa asilimia 80 ya waliohojiwa walitaka kubaki na TANU yao huku asilimia 20 wakisema inatosha, lazima vije vingi ili kuiamsha TANU usingizini, lakini na jinsi Dunia ilivyokuwa inabadilika.
Kulikuwa na wimbi la mabadiliko duniani, ambalo lilimshitua Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliyesema hata kama wengi wanataka chama kimoja cha siasa kiendelee, lakini wachache nao wasikilizwe, huku muktadha ukitazamwa na kupewa uzito.
Dk. Tulia Ackson, Spika wa Bunge la Tanzania
Hatimaye tukakubaliana, kwamba muda na wakati ni muhimu na kwa wimbi hilo hapana budi kwenda na mfumo wa vyama vingi vya siasa, hivyo mwaka 1992, vyama pinzani vikazaliwa nchini na msisimko wa kisiasa ukatamalaki.
Msisimko huo ulitokana na jinsi watu walivyokuwa wamezoea unyeyekevu na utiifu kwa TANU na sasa kufikiria ni kwa jinsi gani watatokea watu wa kuisema TANU na kuacha nyimbo za ‘zidumu fikra za Mwenyekiti!’
Watu wakajiuliza itakuwaje mtu au kikundi cha watu kiibuke kuipinga Serikali iliyoko madarakani? Likawa jambo gumu, lakini polepole likazoeleka ingawa kwa wengine ikawa kwa shingo upande.
Hata uchaguzi wa kwanza ulipofanyika, mwaka 1995 chini ya mfumo huo mpya, watu wakawa wanawashangaa kina Augustino Mrema, kina John Cheyo kusimama kumpinga Benjamin Mkapa aliyetokana na chama kikongwe nchini- Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Lakini kwa namna yoyote na kama ilivyotarajiwa, Mkapa akaibuka mshindi kwa kuwa chama chake kilichojichimbia nchini kote na kilishazoeleka hawa wengine wakaonekana kama wageni ambao wangeipoteza nchi.
Jambo la msingi la kujifunza ni kwamba mfumo wa vyama vingi ulikuwa sawa kabisa na betri, kwamba bila chanya na hasi kukutana hakuna ambacho kingefanyika, hivyo kukawa na ushirikiano wa aina hiyo kisiasa.
Kwamba Serikali imelala, upinzani unaiamsha kwa hoja na si kutukanana au kupigana, ilikuwa ni katika dhana ya kupingana bila kupigana. Kwa kuwa bungeni kulikuwa na wabunge wa chama tawala na wale wa upinzani, hivyo kukawa na Kiongozi wa Upinzani Bungeni (KUB).
Mussa Zungu
Huyu akawa na mawaziri kivuli ambao walizisemea wizara za Serikali kwa upande wa pili, yaani chanya ikizungumza, hasi inajibu na kukubaliana kimsingi, jinsi ya kuenenda na Serikali chini ya mfumo wa vyama vingi.
Kipindi hicho ndicho kilishuhudia kazi ikifanyika bila kulala, Serikali ikijua ikilala tu, wapinzani wanaweza kuchukua nchi na wao wakahamia kiti cha upinzani, hivyo kazi ikawa kazi kweli kweli.
Mifano ya utendaji na ufanyaji kazi ipo mingi ambayo inaonekana kwa macho kutokana na kibano ambacho Serikali ilikipata bungeni, hususan enzi za utawala wa marais Mwinyi Mkapa na Jakaya Kikwete.
Enzi hizo ndizo ziliruhusu maoni mbadala bungeni na kukosolewa chanya kulikofanywa na wabunge wa upinzani, na kuifanya nchi kufanikisha miradi mingi ya maendeleo. Hiyo ilikabadilika enzi za utawala wa Dk John Magufuli.
Hizo ni enzi ambazo wapinzani walikaliwa kooni kwa kuzuiwa kufanya shughuli za kisiasa, wakiambiwa wasubiri nyakati za uchaguzi, huku mikutano ya Bunge sehemu kubwa ikizuiwa kuoneshwa mbashara kwa madai kuwa ilizuia watu kufanya kazi!
Kibano hicho kilichangia hata kazi za maendeleo kwa wananchi kubanwa na ndiyo sababu katika mitaa mbalimbali mathalan jijini Dar es Salaam, hivi sasa kuna mdororo wa ujenzi na hata ukarabati miundombinu, kutokana na kuwa na Bunge la sasa ambako linaonekana kama la chama kimoja.
Na hiyo imedhihirika hata katika uchaguzi wa Spika wa Bunge wa sasa, Dk Tulia Ackson na Naibu wake, Musa Hassan Zungu, ambapo walishinda kwa kura zaidi ya asilimia 90 kana kwamba hakukuwa na wapinzani.
Si kwamba lazima wapinzani wakatae kila linaloletwa na Serikali, la hasha, ila wapinzani wahatakiwi wakubali kila linaloletwa na Serikali, kama wakiambiwa hili ni bakuli wakatae wakisema ni kikombe ingawa wanajua ni bakuli, kwa maana ya kutaka kuthibitisha lakini ia kufanya marekebisho na kusonga mbele.
Hoja zikiwasilishwa na Serikali si lazima zipite kwa wapinzani bila kufanyiwa marekebisho chanya, ambao baadhi ya watu serikalini hudhani wapinzani ni maadui huku wakijua ni Watanzania wenye haki kama wao.
Upinzani ni nafasi tu ya kufanya mambo yaende, hivyo ushirikishwe katika kujenga nchi na si kubomoa. Dhana kwamba maendeleo hayapelekwi walikochaguliwa wapinzani ni mufilisi.