Dar es Salaam. Chama cha Mapinduzi (CCM) kinatarajia kuitisha mkutano Mkuu maalum wenye lengo la kufanya mabadiliko ya katiba yake ili kuongeza kasi ya ufanisi wa kazi na utekelezaji wa uamuzi ya vikao vya chama hicho.
Taarifa iliyotolewa leo Jumamosi Machi 12, 2022 na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka imeeleza kuwa mabadiliko hayo yanatokana na maazimio ya kikao cha kawaida cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kilichofanyika Desemba 18, 2021, kilichopokea, kujadili na kupitisha marekebisho ya katiba ya CCM ya mwaka 1977 toleo la 2020.
Amesema lengo lingine ni kukiwezesha chama kupata viongozi imara, waadilifi na wenye uwezo mkubwa katika kuongeza na kusimamia majukumu ya Serikali za mitaa kwa ufanisi.
"Lengo lingine ni kuongeza na kuimarisha udhibiti wa chama na viongozi wake wanaochaguliwa na kuongoza kusimamia utekelezaji wa ilani ya CCM kupiti Serikali za mitaa," amesema.
Aidha amebainisha kuwa mamlaka ya kupitisha na kurekebisha katiba ya CCM, yapo mikononi mwa mkutano Mkuu Chini ya ibara ya 99 (5) ya katiba ya chama ya mwaka 1977 toleo la 2020.
Amesema Kamati kuu imeazimia kuwasilisha kwa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa pendekezo la kuitishwa kwa mkutano mkuu maalum wa CCM Taifa.
"Machi 31, 2022 Kamati Kuu ya CCM itakutana na Kufuatiwa na Halmashauri Kuu ya Taifa siku hiyo hiyo. Aprili Mosi, 2022 Mkutano Mkuu wa CCM Taifa na vikao vyote vilivyotajwa vitafanyika Makao Makuu Dodoma," amesema Shaka.