Chadema Kanda ya Ziwa Wamtaka Mbowe Aanzie Alikokamatwa




Mwanza. Uongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Ziwa Victoria umesema kuachiwa huru kwa Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho ni ushindi.

Akizungumzia hatua ya Ofisi ya Taifa ya Mwendesha Mashtaka (DPP) kuwasilisha nia ya kutotaka kuendelea na kesi hiyo leo Machi 4, Katibu wa Chadema Kanda ya Victoria, Zakaria Obadi amesema ilikuwa ni suala la muda tu kiongozi huyo wa upinzani kuachiwa kwa sababu tangu mwanzo kesi hiyo ilionyesha kuwa na uelekeo wa kisiasa kuliko jinai.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu, Obadi ametaja funzo lingine inayoambatana na Mbowe kuachiwa huru kuwa ni umuhimu wa mamlaka zinazohusika na kesi za jinai kufanya uchunguzi wa kina na kukusanya ushahidi unaojitosheleza kabla ya kufungua shauri mahakamani kuwaepusha wasio na hatia kusota mahabusu kwa kesi zisizo na dhamana.

Ziara ya kwanza ya Mbowe

Akizungumzia shughuli ya kisiasa ya Mbowe baada ya kuachiwa huru, Obadi amesema uongozi wa kanda ya Ziwa Victoria unawasiliana na ule wa Taifa kushawishi kazi ya kwanza ya kisiasa ya Mwenyekiti huyo ifanyike jijini Mwanza alikokamatiwa wakati wa maandalizi ya kongamano la katiba.


“Mwenyekiti Mbowe alikamatwa zaidi ya siku 200 zilizopita akiwa jijini Mwanza wakati wa maandalizi ya kongamano la katiba; tunawashawishi wenzetu wa makao makuu aanzie kazi Mwanza baada ya kutoka mahabusu alikoshikiliwa kwa miezi kadhaa,” amesema Obadi

Amewaasa viongozi, wanachama, wafuasi na wapenzi wa Chadema kote waliko wajitokeze kwa wingi kuchangia kiwango chochote walichonacho kupitia kampeni ya “shilingi yetu, nguvu yetu na Chadema dijitali” ili kukiwezesha chama hicho kikuu cha upinzani nchini kumudu gharama za kujiendesha bila kutegemea ruzuku kutoka serikalini.

Akizungumzia kuachiwa kwa Mbowe, Martine Malima, mkazi wa jiji la Mwanza amesema; “Mama (Rais Samia Suluhu Hassan) anaupiga mwingi. Naamini Watanzania tutaendelea kushuhudia na kupata mengi kutoka kwa mama,”


Akifafanua, Malima anasema kufutwa kwa kesi ya Mbowe ilikuwa ni ombi na ushauri kutoka kwa watu wa kada na makundi mbalimbali ya kijamii, hivyo utekelezaji wake ni ushahidi kuwa Taifa limepata kiongozi msikivu na anayefanyia kazi hisia, ushauri na maoni ya wananchi kwa misingi na taratibu za kisheria.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad