KUSUKA au kunyoa kwa wabunge 19 wa Viti Maalumu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo ‘Chadema’ uamuzi wake upo mikononi mwa Baraza Kuu la chama hicho litakaloketi mwezi ujao.
Hayo yamewekwa wazi na baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu (majina kapuni) iliyoketi juzi kujadili mambo mbalimbali yahusuyo chama hicho ikiwemo suala la hatma ya wabunge hao 19 wanaotuhumiwa kutumia njia isiyo sahihi kupata nafasi hizo.
“Tumeazimia jambo hilo likajadiliwe na Baraza Kuu kwa sababu sisi Kamati Kuu tulishaamua na watuhumiwa walikata rufaa.
“Rufaa yao itajadiliwa na Baraza Kuu, tulichokubaliana ni kwamba baraza likibarki kufukuzwa kwao tutalazimika kama chama kuchagua wanawake wengine ambao watakwenda kuchukua nafasi za hao 19 za viti maalumu vya Chadema.
“Utakumbuka mwanzo tulikuwa tumegomea kupeleka mbunge yoyote, lakini sasa maazimo yetu siyo hayo, tumelegeza msimamo katika kujenga nchi,” alisema mjumbe mmoja ambaye hakupenda kutajwa jina kwa sababu siyo msemaji wa chama.
Wabunge 19 wanaotuhumiwa kwenda kinyume na msimamo wa chama hicho ni: Halima Mdee, Esther Matiko, Grace Tendega, Cecilia Pareso, Ester Bulaya, Agnesta Lambart, Nusrati Hanje, Jesca Kishoa na Hawa Mwaifunga.
Wengine ni Tunza Malapo, Asia Mohammed, Felister Njau, Nagenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda na Kunti Majala.
Stella Fiao, Anatropia Theonest, Salome Makamba na Conchesta Rwamlaza wote wamekuwa katika msuguano na chama chao ambacho ndicho kinachowapa uhalali wa kuwa wabunge.
Endapo Baraza Kuu litabariki uamuzi wa Kamati Kuu wa kuwafukuza uanachama wabunge hao, watakuwa wamepoteza sifa za kuwa wabunge na nafasi zao zitatakiwa kujazwa na wanachama wengine sawa na muongozo wa Tume ya Uchaguzi unavyoelekeza.
STPORI NA RICHARD MANYOTA | GPL