POLISI Mkoa wa Pwani wamesema uchunguzi wa awali wa chanzo kilichosababisha ajali iliyomuua Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Kampasi ya Dar es Salaam, Prof. Honest Ngowi (55) ni uzembe wa dereva la lori.
Prof. Ngowi alifariki dunia mapema leo, baada ya gari alilokuwa akisafiria kuangukiwa na kontena lililokuwa limebeba madini ya shaba. Ajali hiyo ilisababisha magari matatu kugongana.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Kamanda wa Polisi Mkoa Pwani, ACP Pius Lutumo, alisema katika ajali hiyo watu wawili walifariki na wawili walijeruhiwa.
Alisema chanzo rasmi cha ajali hiyo bado kinachunguzwa, hata hivyo uchunguzi wa awali unaonesha ni uzembe wa dereva wa Lori aina ya Scania kuhama upande wake wa barabara na kuigonga Noah, hivyo kusababisha kontena kuchomoka na kuliangukia gari la Prof. Ngowi.
Alisema tukio hilo lilitokea eneo la Miwaleni, Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Vijjini na kusababisha kifo cha Mhadhiri huyo na dereva wake, Innocent Mringo (33), mkazi wa jijini Dar es Salaam.
Aliwataja majeruhi kuwa ni dereva wa lori, Raymond Kimaro (39), mkazi wa Ubungo, Dar es Salaam na Abdallah Mohamed (33) mkazi wa Dar es Salaam, ambaye alikuwa anaendesha gari aina ya Noah.
"Gari namba T 608 AGV likiwa na tela lenye namba T 317 AQM aina ya Scania, likiendeshwa na Raymond Kimaro, likitokea nchini Kongo kwenda Dar es Salaam, lilihama upande wake wa barabara na kugonga gari namba T 256 CMF, aina ya Noah iliyokuwa ikitokea Dar es Salaam kwenda Morogoro.
“Na kusababisha kontena kuchomoka na kuangukia gari SU 38223, aina ya Toyota Land Cruiser, lililokuwa likitokea Dar es Salaam kwenda Morogoro, ikiendeshwa na Innocent Mringo, likiwa na Profesa huyo," alisema Lutumo.
Alisema mwili wa marehemu Prof. Ngowi, umehifadhiwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani ya Tumbi na mwili wa marehemu, Innocent Mringo umehifadhiwa kituo cha afya Mlandizi.
"Majeruhi wametibiwa na hali zao ni nzuri, huku dereva wa lori anashikiiwa na Jeshi la Polisi. Tunawatahadharisha watumiaji wote wa barabara hususani madereva wa vyombo vya moto kuwa makini na kufuata sheria za usalama barabarani, ili kuepusha ajali zınazosababishwa na uzembe,"alisema Lutumo.
Naye mdogo wa marehemu, Juvenalis Ngowi kwa sasa wanawasiliana na familia na mwajiri wake, ili kujua taratibu za mazishi.