Dar es Salaam. Mwanamuziki nyota wa pop nchini, Diamond Platnamuz amemjibu msanii mwenzake aliyekuwa kampuni ya Wasafi, Harmonize kuhusu tuhuma za unyonyaji na njama za kushusha wengine, lakini akahimiza jitihada na kujiamini ili Watanzania waliteke soko la kimataifa.
Diamond alikuwa akizungumza katika kipindi cha The Switch cha Wasafi FM jana jioni baada ya kuachia albamu yake ya kidigitali au EP.
Katika kipindi hicho, watangazaji walimuuliza nyota huyo wa miondoko ya Bongo Fleva kuhusu tuhuma alizotoa Harmonize, ambaye alidai kuna njama za lebo hiyo kuwashusha wasanii wanaoanza kuwika, maneno aliyosema mara tu alipotua nchini akitokea Marekani mwaka jana.
Bosi huyo wa Konde Music WorldWide pia alisema mikataba mingi ya Wasafi na wasanii ni ya kinyonyaji.
Kuthibitisha hoja zake, Harmonise aliwasikilizisha waandishi wa habari mazungumzo yake na sauti aliyodai ni ya Rayvanny kuonyesha jinsi asivyoridhishwa na mambo ya Wasafi, jambo lililoibua ubashiri kuwa nyota huyo wa "Kwetu" pia yuko mbioni kujiengua Wasafi.
"Sikufuatilia kusikiliza. Unajua huwezi kumzuia mtu kuongea anachotaka kuongea," alisema Diamond.
"Kuhusu WCB au Wasafi, hatuna mikataba wala system yetu si ya kumshusha mtu wala unyonyaji. Huwa nawaambia wanamuziki, ukienda dunia nzima, lebo ya Wasafi nadhani ndiyo inafavour sana wasanii kwa sababu inafanywa na msanii. Sikuwa naangalia favour, bali heshima kwanza kwa sababu msanii akifanikiwa..."
"Mvulana kutoka Tandale" alishauri wenye kampuni za kurekodi muziki wawe mfano wa kusaidia wasanii ili wafanikiwe, badala ya kulaumu wengine.
Diamond pia alisema haumii anaposikia anasemwa vibaya.
"Ikitokea mtu akanizungumzia vibaya, of course, zamani nilikuwa naumia sana, lakini sasa hivi napuuza, halafu naona kwangu mimi ni baraka kwa sababu akinizungumzia vibaya wakati kitu sijakifanya, Mwenyezi Mungu ananibariki, yaani nakuwa nabarikiwa zaidi," Mkali huyo wa kibao cha "Nana".
Diamond alisema haamini katika kumshusha mtu kimuziki ili yeye afanikiwe, bali kujiamini ndio silaha ya mafanikio.
Alisema milango mingi ipo wazi, ila kinachotakiwa ni kujituma na ubunifu, akitoa mfano wa wimbo wa "Sukari" wa Zuchu, ambao alisema umevunja rekodi aliyokuwa anaishikilia ya kuwa na namba kubwa katika YouTube kuliko kazi ya Mtanzania yoyote kwa sasa.
"Kwa hiyo naamini kila mtu anaweza kufanya kitu... mtu huwezi kukaa siku nzima unasikiliza wimbo wangu tu. So, siamini katika kumfanyia mtu figisu, sipendagi noma na mtu," alisema.
Baadaye aligeukia ushauri kwa wasanii wengine, akitaka wafanye kazi kuiteka dunia.
"Tuna nafasi kubwa sana ya kwenda mbali. Tusifocus kwanza kwa Diamond, Diamond. Kwa sababu mimi mwenyewe huko niliko wanaona niko peke yangu. Watu wafanye research wachunguze nimewezaje kufika nje. Yaani milango iko wazi. Ukifocus Diamond, Diamond utashindwa kuvuka," alisema.
Kwa sasa Diamond, ambaye alichomoza kimataifa na video ya "Number One aliyoshirikiana na Mnigeria Dovido, anaitangaza albamu yake ya kidigitali aliyoipa jina la FOA, ikimaanisha awali ya yote (First of All).