Donald Trump Aibuka, Ampinga Vikali Putin




RAIS wa zamani wa Marekani, Donald Trump ameibuka kwa mara ya kwanza na kuzungumzia vita inayoendelea baina ya Urusi na Ukraine ambapo amepinga vikali hatua ya Rais Vladimir Putin kuivamia Ukraine.


Trump amesema alimchukulia kawaida Putin alipoanza kupeleka vikosi vya majeshi mpakani mwa Ukraine akiamini ilikuwa ni kwa lengo la kutengeneza mazingira ya majadiliano baina yake na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy.


Katika mahojiano aliyoyafanya na Gazeti la Washington Examiner la Marekani kwa njia ya simu, Trump amesema ameshangazwa na hatua ya Putin ya kuivamia Ukraine.


“Imenishangaza. Nilifikiri ilikuwa ni mbinu ya majadiliano baada ya Putin kupeleka vikosi kwenye mipaka ya nchi yake na Ukraine na nadhani ilikuwa ni njia ngumu lakini ilikuwa ni nzuri kwa kufanyia majadiliano,” amenukuliwa Trump.


Trump ambaye alikuwa na uhusiano wa karibu na Putin wakati wa utawala wake, amedai kwamba Putin amebadilika sana tangu wawili hao walipofanya kazi pamoja.


Rais huyo wa zamani wa Marekani, amekuwa akikosolewa vikali kutokana na namna anavyomchukulia Putin hasa anavyoshindwa kutamka na kukemea hadharani kitendo cha Putin kuivamia Ukraine.


Makamu wa Rais wa Zamani wa Marekani, Mike Pence pamoja na mshauri wa zamani wa usalama wa taifa kutoka Ikulu ya Marekani, Robert O’Brien ambao wote ni wanachama wa chama cha Republican, kwa pamoja wamekemea kitendo cha Putin kuivamia Ukraine na kueleza kwamba ndani ya chama chao hakuna nafasi kwa wale wote wanaomuonea huruma au kumuunga mkono Putin.


Jumanne ya wiki hii, Trump alikanusha madai kwamba wakati wa utawala wake, hakuwa mkali kwa Rais Putin kutokana na ukaribu aliokuwa nao.


“Nilikuwa mkali kwake, sikuwa mrahisi hata kidogo lakini hata hivyo nilikuwa naye karibu na hilo halishangazi kwani nilifanikiwa kuwa karibu na viongozi wengi duniani,” alinukuliwa Trump.


Wakati huohuo, taarifa kutoka White House zinasema Machi 24, 2022, Rais wa Marekani Joe Biden anatarajiwa kufanya ziara yake ya kwanza barani Ulaya tangu kuanza kwa vita ya Urusi na Ukraine, lengo kuu la ziara hiyo ikiwa ni kujadiliana na NATO kuhusu mustakabali wa Ukraine.


Lakini pia Jumatano ya Machi 16, 2022 Rais Biden anatarajiwa kutangaza nyongeza ya kiasi cha fedha cha dola milioni 800 kwa ajili ya kusaidia usalama wa Ukraine.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad