EDO Kumwembe "Pamoja na Kuwa Ana Homa ya Vipindi Goli la Morrison Litaibeba Simba CAF

 


TUANZE na pambano lenyewe uwanjani? Nadhani halina maana sana. Mpaka sasa ni bao la Bernard Morrison tu pale Niger ndilo ambalo linaifanya Simba kuwa timu pekee iliyofungwa mechi moja katika kundi lake la D.

Vinginevyo kila timu katika kundi hili imeshinda mechi mbili nyumbani na kufungwa mechi mbili ugenini. Ni kasoro Simba tu. Haishangazi kuona ndio maana Simba wanaongoza kwa pointi moja wakiwa na pointi saba halafu Asec na Berkane wana pointi sita.


Ina maana kwamba zile pointi mbili ambazo Gendermarie wamepoteza nyumbani dhidi ya Simba ndizo ambazo zimeshusha pointi zao kutoka sita kwenda nne. Kama Bernard asingefanya yake basi kila timu ingekuwa imeshinda mechi mbili nyumbani na kufungwa mechi mbili ugenini.


Ina maana msimamo wa kundi hili ungeonyesha kwamba kila timu ina pointi sita. Wangekuwa wanapishana idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa. Hii maana yake nini? Mpira wa Afrika timu huwa zinashinda nyumbani na kufungwa ugenini.


Walinishangaza Berkane. Nao juzi walikuwa uwanja wa Mkapa wakiendeleza utamaduni huu. Simba hawakunishangaza sana. Uwanja wao wa Mkapa ni wa kujidai. Ni wale Makhirikhiri kutoka Gaborone ndio ambao waliharibu utamaduni huu.


Afrika ndani ya klabu moja kunakuwa na timu mbili. Berkane waliocheza kwao Morocco wiki chache zilizopita sio hawa waliocheza Dar es Salaam. Simba waliocheza Morocco wiki chache zilizopita sio Simba hawa wa juzi.


Berkane hawakuweza kupiga pasi sita, walikuwa hawana mikimbio kuelekea katika lango, walionekana kuwa wazito na sio wenye kasi kama wale ambao tuliwaona wakiwa tishio nyumbani wiki chache zilizopita.


Simba nao wakabadilika. Walionekana kuwa wepesi na wanaotaka mambo yatokee. Ousmane Sakho akafunga bao la juhudi binafsi lakini ambalo usingeweza kusema kwamba Simba walikuwa wanategemea juhudi za mchezaji mmoja mmoja. Kabla ya hilo bao na baada ya hilo bao Simba walikuwa timu bora uwanjani na hata namba zilionyesha.


Kulikuwa na matukio mawili matatu uwanjani. Sadio Kanoute alistahili kadi nyekundu kwa ujinga alioufanya. Berkane walistahili penalti kwa faulo ya Aishi Manula. Siku nyingine awe makini zaidi uwanjani kwani rafu ile ingeweza kubadili kila kitu.


Berkane pia walistahili kupewa bao ambalo lilikataliwa na mwamuzi wa pembeni kwa madai mfungaji alikuwa ameotea. Ni kweli kulikuwa na wafungaji wengi wa Berkane waliokuwa wameotea lakini mfungaji hakuwa ameotea.


Katika matukio yote ambayo yalikwenda vibaya dhidi ya wageni hili unaweza kumsamehe mwamuzi wa pembeni. Kundi kubwa la wachezaji wa Berkane walionekana kuotea. Ilikuwa vigumu kwa mwamuzi. Hata leo tunaandika haya baada ya kupitisha rula kupitia video mbalimbali. Hata kwa Wazungu wangegundua uhalali wa bao lenyewe kwa kupitia Var.


Na sasa kundi la Simba limesimama kama lilivyo kukiwa na pointi saba, sita kwa wawili na nne kwa mmoja. Ina maana hili kundi linaweza kuamuliwa mwishoni kabisa. Tukifuata mpangilio ulivyo tunaweza kusema Simba itafungwa na Asec halafu Gendermarie itaichapa Berkane pale Niger.


Hadithi ya kufikirika ni kwamba kufikia hapo Asec itakuwa na pointi tisa, Simba itabakiwa na pointi saba, Gendermarie watakuwa na pointi saba na Berkane watakuwa na pointi sita.


Lakini mechi za mwisho Simba itashinda dhidi ya Gendermarie Uwanja wa Mkapa na hivyo kufikisha pointi kumi, Berkane wataichapa Asec pale Morocco na kufikisha pointi tisa sawa na Asec wenyewe, wakati Gendermarie atabakiwa na pointi saba.


Hii ina maana bao la Morrison ugenini litakuwa bao muhimu kwa Simba mwisho wa msimu. Nimeandika hadithi ya kufikirika kutokana na namna ambavyo timu za Afrika zinashinda nyumbani na kufungwa ugenini. Inaweza isitokee lakini mpira wa Afrika unashangaza zaidi jinsi ambavyo mbabe analowa zaidi akiwa ugenini.


Bila ya kujali lolote ambalo linaweza kutokea nyumbani kwa Asec ukweli ni kwamba Simba wanahitaji kushinda pambano lao la mwisho Uwanja wa Mkapa. Ni kazi ambayo wanaweza kuifanya. Ni nadra sana kwa timu kufikisha pointi kumi katika kundi lake halafu isifuzu.


Kitu kilicho wazi zaidi ni kwamba Simba wanahitajika kuimarika katika hatua za mbele. Bado kiwango chao sio kikubwa sana kulinganisha nyakati zile ambazo walikuwa wanawalalisha mapema wakubwa wa soka la Afrika kama Al Ahly na AS Vita.


Kuna baadhi ya wachezaji wa Simba wana homa za vipindi. Hawa ndio hasa ambao walipaswa kuishika timu. Morrison, Sakho na Rally Bwalya. Wachukue muda kutazama mikanda ya Clatous Chama na Luis Miquissone wakati ule wakiisaidia Simba kuchanua zaidi katika michuano ya Afrika. Walikuwa na viwango bora kila wakati.


Mchezaji kama Morrison sio wa kutokea benchi kama Chama na Miquissone hawapo tena. Hata hivyo bado anatokea benchi. Kocha wake sio mjinga. Kuna kitu anakiona hakipo sawa. Leo Morrison anakuwa shujaa, keshokutwa anakuwa ovyo.


Upande wa ulinzi Simba wapo imara chini ya Joash Onyango na Henock Inonga. Upande wa kulia Shomari Kapombe amekuwa na kiwango kizuri hivi karibuni huku Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ akiwa nyota zaidi kwa sasa klabuni.


Washambuliaji itabidi warudishe makali, lakini zaidi Kibu Dennis anaweza kuwasaidia zaidi Simba kama akiendelea kuwa fiti.


Ametoka katika majeraha ambayo yalimuweka nje kwa muda mrefu kidogo. Akiendelea kupata mechi akarudisha kasi yake atawasaidia Simba katika kutengeneza mashambulizi kutokana na kasi, lakini pia kutupia.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad