Halmashauri ya mji wa Geita imeiomba Jumuiya ya Serikali za Mitaa nchini (ALAT) kupeleka kilio chao kwa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ili warudishiwe gari lao la kifahari lililochukuliwa na Serikali kwa madai ya kununuliwa kwa bei kubwa.
Gari hilo aina ya Toyota Land Cruiser V8, lilichukuliwa na TAMISEMI mwishoni mwa mwaka 2020 kufuatia malalamiko ya Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Musukuma kuwa gari hilo lilinunuliwa kwa bei kubwa ya Sh 400 milion bila ridhaa ya madiwani, wakati huo akidai kulikuwa na upungufu wa vyumba vya madarasa na vituo vya afya.
Kutokana na tuhuma hizo, Desemba 2020 aliyekuwa Rais wa awamu ya tano, Hayati John Magufuli aliagiza kusimamishwa kazi kwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji, Modest Apolnary, kwa matumizi mabaya ya fedha za umma.
Hata hivyo, akizungumza leo Machi Mosi katika ziara ya viongozi wa ALAT taifa waliotembelea halmashauri hiyo, Mwenyekiti wa halmashauri ya mji, Constantine Morandi amesema wameandika barua kadhaa kudai gari hilo, lakini badala yake wamepatiwa gari jingine ambalo halilingani na thamani ya fedha ya awali.
“Badala ya kurudisha gari letu walitupa gari jingine ambalo sio jipya na limetembea kilometa 100,000 na hata bei yake sio ile. Basi waturejeshee fedha zetu au warejeshe gari lilelile,” amesisitiza Morandi.
Amesema taarifa za gari zilizotolewa zilikuwa za upotoshaji kwa kuwa baraza hilo kabla ya kuvunjwa liliridhia na taratibu zote za manunuzi zilifuatwa.
“Mamlaka za juu hazikushauriwa vizuri juu ya ununuzi wa gari lile, zile zilikua fedha za mapato ya kodi za wananchi wa mji wa Geita na hazikua fedha za CSR (huduma za jamii) na baraza lilitoa baraka zake kabla halijavunjwa.
Akijibu maombi hayo, Mwenyekiti wa ALAT Taifa, Murshid Mgeze amesema watalifuatilia gari hilo kwa kuwa halmashauri ni taasisi inayojitegemea na ina mali zake.
geitapic
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa (ALAT), Murshid Mgeze akizungumza wakati waliotembelea halmashauri ya mji wa Geita kwa lengo la kuona miradi inayotekelezwa na halmashauri hiyo kwa fedha zilizotolewa na Serikali
Alisema kwa kuwa gari lilinunuliwa na mapato ya ndani ya halmashauri watalazimika kuonyesha fedha hizo zilivyotumika.
“ALAT hatupendi halmashauri iwe na hati chafu, mkipata hati chafu na sisi tunapata doa msiporudishiwa gari au mkarudishiwa kiasi cha fedha basi wakaguzi wakikagua lazima muwe na hoja za kujieleza ambazo mkishindwa mtajikuta na hati chafu kitu ambacho hatutaki kitokee,” amesema Mgeze.
Novemba 2020, Mbunge wa Jimbo la Geita Vijijini, Joseph Kasheku maarufu Musukuma alimtumia salamu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Geita kufuatia halmashauri hiyo kufanya manunuzi ya magari likiwemo Gari la Mkurugenzi Toyota V8 lenye thamani Sh. Milioni 400 ambapo alidai manunuzi hayo ni ya zaidi matumizi mabaya ya fedha za umma.
Musukuma alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na Waadishi wa habari Mkoani Geita ambapo alidai kununua gari hiyo ni kwenda kinyume na matumizi ya fedha za SCR zinazotolewa na Mgodi wa Dhahabu wa Geita GGML.