Golikipa Mwameja "Ishu ya kuuza matikiti Uingereza Nilipoenda Kufanya Majaribio iko hivi"



Wengi wamesikia au kuhadithiwa habari ya Mwameja kuuza matikiti nchini Uingereza ambapo hapa nchini ilielezwa kuwa alikwenda nchini humo kwa ajili ya majaribio kwenye timu ya Reading mwaka 1996.

Hata hivyo katika mahojiano maalumu na Mwanaspoti yaliyoanza jana, kipa huyo wa zamani wa Simba anasema hakuna maisha ambayo atakuja kuyasahau kama yale aliyoishi nchini humo ambapo hapo ndipo ugomvi wake na Muhidin Ndolanga, mwenyekiti wa zamani wa FAT (sasa ni marehemu) ulipoanzia.

“Nilisikia taarifa hizo kwamba niko kule nauza matunda na mambo kama hayo kwa kuwa kweli sikuwa na ishu kule, ila yote niliyavumilia. Ndiyo sababu mwanzo nilisema kuna maneno ya watu wa mpira unapaswa kuwa na roho ngumu sana kuyavumilia.

“Ingawa kiukweli maisha yangu ya Uingereza yalikuwa magumu tena sana, lakini ni kwa sababu ya watu wa FAT (sasa TFF) na hapo ndipo mgogoro wangu na Ndolanga ulipoanzia,” anasema.


Anasema safari yake ya Uingereza ilianzia akiwa timu ya taifa ambayo ilicheza mechi na Zimbabwe na ndipo alikutana na wakala, raia wa Afrika Kusini, Jomo Sono, ambaye sasa ni mmiliki wa klabu ya Jomo Cosmos.

“Aliniona kwenye ile mechi. Baadaye akanifuata tukazungumza. Baada ya siku kadhaa nikaenda Afrika Kusini tukaingia mikataba akanieleza lengo ni kunipeleka Ulaya kwenye majaribio. Tulikubaliana nikarudi Tanzania kujiandaa na safari,” anasema Mwameja.

Anasema kabla ya safari ya Uingereza alimuomba wakala huyo ambaye pia ni gwiji wa soka wa Afrika Kusini pesa kidogo kwenye mkataba wake kwa ajili ya maandalizi ya safari.


“Ile pesa dola 700 ilitumwa FAT, wakati wa Ndolanga na Rage (Ismail Aden) akiwepo FAT. Nikaitwa na viongozi wakati huo ofisi za FAT zilikuwa Kisutu na Mwenyekiti wa Simba, mzee Abdallah Kipukuswa alikuwepo katika kikao kile.

“Niliambiwa kuna pesa inatakiwa upewe kwa ajili ya safari, lakini sisi tunaidai klabu yako ya Simba na kwa kuwa wewe ni mali ya Simba basi sisi tumechukua hiyo hela ili kufidia deni tunaloidai klabu yako. Hivyo sikupewa ile pesa na ndiyo tofauti yangu na Ndolanga ilivyoanza.

“Walisema mimi ni mali ya Simba, mkataba wangu na Jomo pesa wakachukua wao. Ilikuwa ni changamoto sana kwangu, muda wa safari ulifika sina pesa, nikachelewa kama wiki moja ila niliondoka nchini kwa pesa yangu lakini kwa kuchelewa.

“Ilikuwa ni safari ngumu sana kwangu, kufika kule nikafuzu majaribio, ila kucheza ikawa ngumu sababu sikuwa na ITC na kuipata ikawa ni shida, yule wakala akaniambia nirudi Tanzania ili nianze upya.


“Nikiwa Uingereza nikampigia simu Nicco nikamueleza kwa changamoto ninazopitia kuna mtu mmoja anaitwa Abubakar pia nilimueleza bora nirudi nyumbani, akaniambia hapana hebu subiri tuone tunafanyaje.”

Anasema wakati ule tayari alishapata meneja ambaye aliitwa Mr Member na timu ya Reading ilitaka kumtumia Mwameja lakini ITC ilikuwa kikwazo.

“FAT wakadai wameituma ITC yangu nchini Afrika Kusini. Nikawaomba basi niandikieni barua ya kunitambua tu, lakini pia walikataa. Kiukweli sikushindwa ila nilisababishiwa na watu kushindwa,” anasema.

Anasema ilifikia hatua wale wenyeji wake wakataka watumie njia ya mkato ili acheze soka kwenye timu ile, lakini aliwaambia hapana.


“Siku narudi nchini sikuwa na morali kabisa ya kucheza mpira. Niliona kama nimerudishwa nyuma hatua kubwa na watu sababu tu ya dola 700 ambayo ilikuwa ni haki yangu. Wapo ambao walinishauri niende kwenye vyombo vya sheria, lakini sikuona sababu ya kufanya hivyo.”

Anasema hataisahau safari ya kurudi nchini hasa akikumbuka alivyoishi katika mazingira magumu akiwa nje ya nchi kwa sababu ya baadhi ya watu.

“Mpira umenifanya nipitie changamoto nyingi, lakini namshukuru Mungu nilipata marafiki wengi sababu ya mpira na maadui wachache sana.

KUFUKUZWA TIMU YA TAIFA

Aliporejea nchini, Mwameja anasema alirudi kuitumikia Simba na kuitwa timu ya taifa iliyoingia kambini kujiandaa na mechi na Misri. “Ilikuwa ni kipindi cha Ramadhan, hivyo kuna baadhi ya wachezaji tuliokuwa tumefunga ikifika muda wa kufuturu tunakwenda kufuturu nyumbani kisha tunarudi kambini, huo ndio ulikuwa utaratibu.

“Kwenye ile mechi tulifungwa bao 1-0. Kwenye ripoti ikaonekana wachezaji hawakuwa kambini, tulikuwa wengi, lakini sababu tayari kulikuwa na tofauti dhidi yangu huko nyuma ikaamuriwa sina nidhamu nikatimuliwa timu ya taifa.”


Anasema bifu lake na Ndolanga liliendelea hadi kwenye moja ya mashindano ambayo Simba ilitwaa ubingwa na yeye kutopeana mkono na mwenyekiti huyo wa FAT wakati alipokabidhiwa kombe kama nahodha.

“Waziri Philemon Sarungi (aliyewahi kuwa mlezi wa Simba SC) alikuwa anajua uhusiano wangu na mwenyekiti sio mzuri aliniita akasema inabidi mmalize tofauti zenu maana timu ikishinda na kuwa bingwa nahodha na mwenyekiti hamuwezi kupeana mkono. Nilimkatalia na hata yeye alijua hilo na kweli ndicho kilitokea.

“Hadi ameondoka (Ndolanga alipofariki) hatukuwa na maelewano mazuri naye,” anasema.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad