MFANYABISHARA Ghalib Said Mohamed maarufu GSM, ametoa vielelezo kadhaa vinavyoonesha kuhusika katika umiliki wa eneo lenye mgogoro baina yake na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).
Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya kusambaa kwa video ambayo Makonda alionekana akidai kuwa eneo hilo ni la kwake huku akiwa amezingirwa na watu akiwemo askari aliyevalia sare za jeshi la polisi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumamosi tarehe 12 Machi 2022, Mwanasheria wa GSM, Alex Mgongolwa, amesema mteja wake amempa maelekezo ya kukanusha umiliki wa Makonda na kuchukua hatua zaidi ikwemo kwenda mahakamani endapo ataendelea kudai eneo hilo ni lake.
“Leo tumewaita hapa ili kuwapa taarifa fupi ya uhalali wa umiliki wa eneo lenye Plot namba 60 lililopo Regent Estate Manispaa ya Kinondoni, Dar Es Salaam,” amesema Mgongolwa.
Mgongolwa amesema Mohammed alinunua ardhi hiyo kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya makazi tarehe 21 Novemba 2006 na kuonyesha waandishi wa habari nyaraka za udhibitisho.
Amesema Tarehe 19 Septemba 2017, Mohammed aliingia Mkataba na Kampuni ya ujenzi iitwayo Group Six International wenye thamani ya Sh 640 milioni “na hii ni nakala ya Mkataba huo.”
Aidha, ameongeza kuwa mteja wake aliomba kibali cha ujenzi na Manispaa ya Kinondoni walitoa kibali cha ujenzi tarehe 16 Oktoba 2017 chenye kumbukumbu namba 00020032 kwa Ghalib Said Mohammed kwa ajili ya kuanza ujenzi wa eneo hilo.
“Baada ya kibali kutolewa, Group Six walianza ujenzi na walipeleka maombi ya malipo ya awali ya ujenzi tarehe 31 Januari 2018 na Ghalib Said Mohammed alitekeleza sehemu ya Mkataba kwa kulipa kiasi cha Sh 51.9 milioni na kuna kithibitisho cha risiti ya TRA,” amesema.