Hamad Rashid aikosoa Chadema, amtaja Mbowe na Lissu




MWENYEKITI wa Chama cha ADC, Hamad Rashid amewapa neno wanasiasa wanaokataa kushiriki shughuli za kiserikali na vikao vya kisheria, akisema Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, alihimiza kushiriki kwani hutoa fursa ya kupata majibu ya changamoto zinazokuwepo. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Rashid ametoa kauli hiyo leo Jumamosi, tarehe 19 Machi 2022, akihutubia katika kongamano la tathmini ya mwaka mmoja wa Rais Samia Suluhu Hassan, madarakani, lililofanyika jijini Dodoma, ambapo mgeni rasmi alikuwa Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson.

Ni siku moja baada ya Chadema, kupitia Mwenyekiti wake Taifa, Freeman Mbowe, kutangaza azimio la chama hicho kutoshiriki kongamano la haki, lililoandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), kikidai halina nia ya kujadili namna ya upatikanaji katiba mpya.

“Nimekuwa naibu waziri wa mambo ya ndani, nikiwa na miaka 32, Mwalimu akasema siku yoyote unapoitwa katika shughuli ya kiserikali, kikatiba, kisheria, usiache kwenda, iwe unataka au hutaki, maana unapokwenda utapata fursa ya kufanya kile ambacho unacho,” amesema Rashid.


 
Katika hatua nyingine, Rashid amehoji watu wanaomkosoa Rais Samia kuwa wanataka nini, ikiwa kiongozi huyo anajitahidi kutatua changamoto zilizojitokeza kwenye utawala uliopita.

Mwenyekiti huo wa ADC, amesema, kutokana na nia ya Rais Samia kurudisha siasa za maridhiano, aliamua kumfutia mashtaka ya ugaidi Mbowe na walinzi wake watatu, Halfan Bwire Hassan, Adam Kasekwa na Mohammed Abdillah Ling’wenya.

Pamoja na kuzungumza na Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, Tundu Lissu, nchini Ubelgiji.


“Juzi ndugu Mbowe baada ya mahakama kusema ana shauri la kujibu, mama akasema hapana, mtu mzima ni mtu mzima, akasema futeni kesi. Huo ni utawala bora, mnataka nini?” amesema Rashid.

Rashid amesema “Rais Samia ameenda ziara Ubelgiji, akasema hapa kuna kijana wetu nikamuone, niambieni ni kiongozi gani duniani ametoka akaenda kumuona mtu aliyeikimbia nchi akazungumza naye? This is Samia. All we are human being, but Samia is Human.”

Mwanasiasa huyo mkongwe nchini Tanzania, amesema Rais Samia anaiongoza nchi kwa kuzingatia utu, ndiyo maana ametoa muelekeo wa namna ya uendeshaji wa demokrasia nchini, kwa kuagiza uundwaji wa kanuni za kusimamia mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa.

“Tulipoenda kumuona Rais Samia Ikulu , akasema jambo la kwanza kuhakikisha vyama vinafanya mikutano yao bila matatizo yoyote. Leo ruhusa ya vyama vya siasa kinachobaki ni kuboresha kanuni, ametoa agizo kwamba hakuna siasa za kutukanana tushindane kwa hoja,” amesema Rashid.


 
Kongamano la haki lililoandaliwa na TCD, linatarajiwa kufanyika mwishoni mwa Machi 2022, jijini Dodoma, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais Samia.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad