Harmo: Nakichafua Muda Wowote



RAJAB Abdul Kahali wengi wanamjua kama Harmonize au Konde Boy Mjeshi; ni staa mwingine mkubwa wa muziki nchini Tanzania ambaye alikuwa ametulia kidogo kupisha upepo wa aliyekuwa bosi wake kunako Lebo ya WCB, Nasibu Abdul au Diamond Platnumz upite kwanza ndipo akichafue.

Harmonize au Harmo alikuwa kimya wakati wote ambapo Diamond au Mondi alikuwa akionesha vurugu zake za uzinduzi wa albam yake fupi (EP) ya First Of All (FOA) iliyoteka hisia za wengi kuanzia wiki iliyopita na wiki hii.

DIAMOND KUTEMA NYONGO
Lakini uzinduzi huo wa FOA haukuishia kwenye uzinduzi tu, bali Diamond alifanya mahojiano na kutema nyongo juu ya mambo mbalimbali huku mengine yakiwa ni vijembe au mafumbo ambayo inasemekana yalikuwa yanamlenga Harmonize hivyo naye anakuja kuyajibu.

Katika mahojiano hayo, Diamond alitupilia mbali madai ya Harmonize kuwa alijaribu kuzuia nyota yake kung’aa. Diamond alisema matamshi ambayo Harmonize alitoa mwaka jana baada ya kutua kutoka Marekani hayana ukweli wowote na yalikosa heshima.


 
Diamond alikana kuwahi kujaribu kumshusha Harmonize au kumwagiza atoe kitita kikubwa cha pesa alipotaka kujitoa WCB.

“Hakuwa na heshima na maneno yake. Sikutaka kufuatilia sana. Kama aliongea hivyo, mimi sikumkataza yeyote kuzungumza anachotaka. Naheshimu maneno yake, naheshimu kama kuna aliyeamini na ambaye hakuamini.

Katika Wasafi, hatuna mikataba au mipango ya kumshusha mtu,” alisema Diamond akijibu tuhuma za Harmonize. Diamond aliweka wazi kuwa, alipokuwa anaanzisha Lebo ya Wasafi (WCB) lengo lake lilikuwa kukuza wasanii wa Tanzania na siyo kumshusha yeyote.

Alisema kuwa, hajalishwi na maneno ya uongo yanayoenezwa na wasanii ambao walitofautiana naye. “Zamani ingetokea mtu aende kunizungumza vibaya, nilikuwa naumia sana. Sasa hivi napuuza, naona kama ni baraka.

“Sikutaka kufuatilia, lakini mwisho wa siku kulizungumzwa. Watu walijua ukweli ni upi na uongo ni upi. Mimi kufikia hatua mpaka kutaka kumdhulumu mtu ama kumshusha, ni ya nini? “Hiyo ni kusema siamini katika mimi.

Mimi naamini katika mimi. Siamini eti lazima nifanikiwe mpaka nimzidi mtu f’lani,” alisema Diamond au Simba wa Tandale. Mbabe huyo wa muziki alimhimiza Harmonize na wasanii wengine kuacha kung’ang’ania ugomvi na yeye katika juhudi za kutafuta kiki kwani hawatamuweza.

HARMONIZE: NAKICHAFUA
Baada ya maneno hayo ya Diamond, habari za ndani zimeeleza kwamba, Harmo amesema;


 
“Nakichafua muda wowote…” Harmonize; jana alitangaza kuanza kukichafua kupitia video yake ya wimbo wake mpya wa Bakhresa ambao ndani yake kila shabiki wake anatamani kuona kuna nini.

Gazeti la IJUMAA limebaini kwamba, audio ya wimbo huo wa Bakhresa hadi jana ilikuwa na zaidi ya wasikilizaji milioni 1.6 katika Mtandao wa YouTube.

TUKIO KUBWA MLIMANI CITY
Mbali na kuachiwa kwa video hiyo ambayo imelenga kuja kuzima vurugu za FOA ya Diamond, kuna tukio kubwa ambalo Harmonize atalifanya keshokutwa Jumapili hii katika Viwanja vya Mlimani City jijini Dar na hapo ndipo mbivu na mbichi zitakapojulikana.

Kwa mujibu wa Harmo, atafanya tukio kubwa linalokwenda kwa jina la One Love Concert kuanzia saa 6:00 hadi saa 12:00 jioni likihusisha walemavu, watoto yatima, akina mama wajane na wengine wote wasiojiweza.

Harmonize anasema kuwa, lengo la tamasha hilo ni kutengeneza furaha ya pamoja kwa kupata chakula cha mchana na kuimba nyimbo zake zote laivu kwenye jukwaa kubwa la wazi.

Harmonize anasema kuwa, anaamini kuwa hiyo ni sehemu ya kurudisha kwa jamii inayomuunga mkono na anaamini litakuwa ni tamasha lenye mguso wa tofauti kwani hakuna msanii aliyewahi kufanya jambo kama hilo ambapo pia anasema kama kuna mwenye swali juu ya muziki wake, basi atapata majibu siku hiyo.

HARMONIZE AWAKARIBISHA WOTE
Harmonize anawakaribisha wote wanaoguswa kuchangia tamasha hilo kwa wahusika ambapo yeye ametoa keshi shilingi miliobni mbili kama kianzio na kwa yeyote anayeguswa anaruhusiwa kushiriki kwa namna yoyote anayoguswa.

Harmonize amesema atakichafua kwelikweli kwa kupiga laivu nyimbo zake zinazokubalika zipatazo 57 na itakuwa ni sherehe kubwa ya kula, kunywa na kupati bila kiingilio kwa yeyote atakayehudhuria.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad