TAARIFA kutoka ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) zinasema hatma ya ubunge wa Halima Mdee na wenzake itafikia ukomo Aprili, mwaka huu.
Watimulliwe au wabakishwe ndani ya chama hicho, uamuzi wake utafikiwa mwezi ujao baada ya Baraza Kuu la Chadema kupitia rufaa yao, chanzo cha ndani kimesema.
Mdee, Esther Matiko, Grace Tendega, Cecilia Pareso, Ester Bulaya, Agnesta Lambart, Nusrati Hanje, Jesca Kishoa na Hawa Mwaifunga wanatuhumiwa kwa utovu wa nidhamu ambao ulisababisha wavuliwe uanachama.
Wengine waliokumbwa na mkasa huo ni Tunza Malapo, Asia Mohammed, Felister Njau, Nagenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda na Kunti Majala.
Wahusika wengine ni Stella Fiao, Anatropia Theonest, Salome Makamba na Conchesta Rwamlaza ambao wote kwa pamoja wanatuhumiwa kujipatia ubunge wa viti maalum kinyume na msimamo wa Chadema uliokuwa umesusia matokeo ya uchaguzi wa 2020.
Mdee na wenzake wamekuwa wakizua sintofahamu kuendelea kuwa wabunge ilhali walishatimuliwa kwenye chama chao, ingawa msimamo wa viongozi wa bunge nao umekuwa ukidai kuwatambua kutokana na mchakato wa kufukuzwa kwao kwenye chama kutofuata misingi ya haki.
Uamuzi wa Baraza Kuu unasubiriwa kutokana na kuwepo kwa rufaa iliyokatwa na Mdee na wenzake baada ya kutimuliwa uanachama na Kamati Kuu na kwamba tetesi za uwezekano wa kamati hiyo iliyoketi jana kuweza kuja na tamko juu yao si za kweli.