NILIGUNDUA mambo machache baada ya kutazama pambano la Berkane dhidi ya Simba juzi usiku pale Morocco. Simba walichapwa mabao 2-0 na walistahili kuchapwa.
Berkane walikuwa katika ubora wao. Sikuwa nimewahi kuwaona kabla lakini wanastahili kufanya vyema michuano hii.
Tumesikia mengi kuhusu kurudi kwa Clatous Chotta Chama. Mwenyewe anasema sababu ni za kifamilia. Wengine wanadai kwamba alishindwa kuendana na mazingira ya maisha ya nchini Morocco. Binafsi nimegundua kitu tofauti kidogo. Ni ndani ya uwanja.
Hawa Berkane wanacheza soka la kasi kwa muda wote. Sidhani kama staili ya Chama ingeendana nao. Labda kama timu ingebadilika kwa sababu yake. Akiwa na Simba Chama anaandaa namna ambavyo timu inapaswa kucheza. Akiwa Berkane hakuwa staa na timu ilikuwa inacheza namna inavyotaka yenyewe.
Berkane niliowaona wana kasi kuliko Chama. Chama anacheza kwa umakini mkubwa lakini taratibu. Kwa soka Simba ni sawa lakini kwa soka la Waarabu nadhani alipaswa kubadilika kidogo. Haishangazi kuona kwamba muda mwingi akiwa Morocco aliutumia kukaa benchi. Naamini Luis Miquissone au Osumane Sakho wangetamba Berkane
Subiri kidogo. Kwanini tuwazungumzie kina Miquissone wakati tuna mfano halisi. Tuisila Kisinda hakuwa mchezaji ambaye tulimthamini sana nchini. Wengi waliamini kwamba alikuwa na kasi kuliko madhara yake. Lakini juzi Tuisila alimaliza dakika zote tisini pale Morocco. Mara nyingi pia amekuwa akianza. Ingawa Chama na Tuisila ni wachezaji tofauti, lakini Tuisila amekuwa akisaidiwa na kasi yake na ndio maana amekuwa akianza. Alikuwa mwiba pia kwa walinzi wa Simba kutokana na kasi yake hii. Ilinikumbusha pia kwamba inawezekana Simon Msuva ametamba Morocco kutokana na staili yake ya soka la kasi.
Kwa soka letu la ndani ni rahisi kwa Chama kuendelea kuwa staa kwa sababu anaamua yeye Simba icheze vipi. Kwa soka la nje inabidi aongeze kasi kidogo. Juzi sikuona mchezaji wa Berkane ambaye angenifanya nione timu yao ilikuwa imefanya makosa kuachana na Chama ndani ya kipindi kifupi.
Mwingine ambaye atapata wakati mgumu kucheza soka la kina Berkane ni pamoja na Rally Bwalya. Licha ya kipaji chake maridhawa, lakini Bwalya anacheza kwa utaratibu na simuoni akiingia katika kikosi cha kwanza cha Berkane kama hata changamka uwanjani.
Tuendelee kujifunza vitu. Unaweza kukuta Kibu Dennis anakwenda kwa Waarabu na akawa staa mkubwa kuliko baadhi ya wachezaji ambao katika ligi yetu tunawaona wana vipaji vikubwa na tumekuwa tukiwaimba kila kukicha. Kitalaamu wanaweza kuwa na udhaifu mkubwa ambao hatuuoni kutokana na kiwango cha ligi yetu.
Tukiachana na habari ya Chama nilichoona kingine ni hiki hapa kwamba Berkane wana kasi kali na Simba pia wanapaswa kujua kuwa mechi ijayo ya marudiano baina ya timu hizi haitakuwa rahisi. Itakuwa fainali kwao lakini wawe makini. Baada ya pambano hili nimegundua kwamba Berkane sio wepesi kama nilivyodhani awali.
Baada ya kutazama pambano hilo nimejiuliza pia namna gani Berkane waliruhusu mabao matatu waliposhinda 5-3 dhidi ya US Gendarmerie. Hapo hapo nimejiuliza kwanini walifungwa na Asec. Wanaonekana kuwa wazuri kuliko Asec na Gendarmerie. Na juzi walionekana kuwa bora kuliko wapinzani wao Simba. Kitu kingine nilichogundua juzi ni mwendelezo wa udhaifu wa Simba katika kucheza mipira iliyokufa (set pieces). Mwanzoni nilidhani Sergi Paschal Wawa alikuwa sehemu ya udhaifu huu, lakini sasa hivi nimegundua kwamba hata walinzi wa sasa wana udhaifu huu.
Bao la pili la Berkane lilikuwa rahisi. Kulikuwa na wachezaji wawili wa Berkane ambao wangeweza kufunga huru achilia mbali mfungaji wa bao lenyewe.
Huu ni mwendelezo tu. Katika mechi mbili walizofungwa mabao 5-0 dhidi ya AS Vita na Al Ahly ugenini Simba waliruhusu mabao haya. Wakati huo Wawa alikuwa katika moyo wa ulinzi lakini hata sasa katika zama za Henock Inonga bado hadithi imeendelea kuwa ileile.
Simba pia waliruhusu mabao mawili ya vichwa walipofungwa 4-0 na Kaizer Chiefs pale Soweto, Afrika Kusini. Ni hadithi ambayo imekuwa ikiendelea. Mipira ya adhabu au krosi imekuwa ikiambatana na mateso makubwa kwa Wekundu wa Msimbazi. Kingine ambacho niligundua ni ukomavu ambao unekuwa ukionyeshwa na mlinda mlango wa Simba, Aishi Manula. Anaitendea haki nafasi yake. Juzi alifanya kosa moja la kitoto lakini kwa ujumla Aishi amekomaa. Anastahili kuwa Tanzania One kwa sasa. Kuna wakati alikuwa anatutia majaribuni kuwafikiria makipa wengine walio bora zaidi yake lakini kwa sasa amemaliza ubishi.
Inatokana na yeye mwenyewe kupevuka kiumri kama inavyokuwa kwa makipa wengi bora duniani, lakini kikubwa zaidi ni kwamba Simba na timu ya taifa wamewekeza kwake kwa kumpatia mechi nyingi za kimataifa ambazo zinamuweka katika misukosuko ambayo inamfanya akomae langoni.
Ni kama vile ambavyo Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na Shomari Kapombe walivyowatangulia wachezaji wengi wa nafasi zao. Ni kwa sababu wamecheza mechi nyingi za kimataifa na Simba pamoja na timu ya taifa katika miaka ya hivi karibuni.