MABOSI wa Simba wanahaha kufanya mazungumzo na baadhi ya wachezaji ambao mikataba yao ipo ukingoni, huku Aisha Manula akiwa miongoni mwa wachezaji hao na kipa huyo amevunja ukimya kuzungumza dili lake la kubaki Msimbazi.
Manula ambaye kiwango chake kimezidi kupanda tangu atue Simba akitokea Azam FC, amezungumza na Mwanaspoti na kuelezea hatma ya mkataba wake ndani ya klabu hiyo na kuanika uamuzi wake mpya.
Manula alisema hawezi kufanya uamuzi wowote kwa sasa, kwani bado ni muajiriwa wa Simba ambayo imekuwa ikimpatia kila kitu ndani ya mkataba wake.
Alisema anafahamu mwisho wa msimu huu anamaliza mkataba na klabu hiyo, ila amewaeleza viongozi wake hatafanya uamuzi mwengine wowote kwani wao ndio anawapa nafasi ya kwanza.
“Naonekana bora zaidi wakati huu kutokana na kupata nafasi kubwa ya kuaminiwa hapa Simba kutokana na mashindano mbalimbali tunayocheza, hivyo kabla ya kuamua chochote juu ya mkataba wangu mpya Simba nimewapa nafasi ya kwanza,” alisema Manula na kuongeza;
“Katika kuhakikisha nakubaliana na Simba nimefanya nao mazungumzo ya kuongeza mkataba mpya na kuna mahitaji nimewaeleza na tumaini langu yataenda sawa na nitaongeza mwingine mpya hapa.”
Manula alifafanua; “Hili jambo la kuja kuongea kabla ya mkataba wangu kufikia mwisho ni heshima kubwa wamenipatia ninaimani kubwa kila kitu kitakwenda vizuri nitakuwa hapa kwa misimu mingine ijayo.
“Sioni nafasi ya Simba kushindwa kuniongezea mkataba mpya kwani wanafanya mambo yao kwa weledi mkubwa ila kama ikitokea hivyo ndio nitafanya uamuzi mwingine ambao kwa sasa sijajipanga nao na sitarajii kama itakuwa hivyo.”
Awali Manula alisaini mkataba wa miaka mitatu uliokuwa na thamani isiyopungua Sh 90 milioni, ikiwa na maana mabosi wa Simba kwa mkataba mpya wanalazimika kutoa mkwanja mrefu zaidi ya huo ili kufanikisha kumbakisha klabuni.
Inelezwa mabosi wa Simba wanapambana kumalizana na Manula kutokana na presha kubwa wanayopata baada ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini kuelezwa inamnyatia kipa huyo aliyeokoa penalti mbili dhidi ya Asec Mimosas katika mechi ya Kundi D ya Kombe la Shirikisho Afrika nchini Benin.
HUYU HAPA TRY AGAIN
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ alisema watambakisha Manula kwa namna yoyote kwani mazungumzo yanaenda vyema na hawajapokea ofa yoyote mezani ya kutakiwa kwake.
Mbali na Manula, wachezaji wengine ambao mikataba yao inamalizika mwisho wa msimu ni; Chriss Mugalu, Meddie Kagere, Hassan Dilunga, Mzamiru Yassin, Joash Onyango, Bernard Morrison na wengineo.