UPANDE wa kushoto wa ulinzi wa Yanga. Yassin Mustafa ameumia. David Bryson ameumia. Shomari Kibwana ambaye huwa anaibia kucheza upande huo, ingawa ni beki wa kulia pia ameumia. Kocha Nasreddine Nabi ameangukia kwa mtu ambaye hatukutazamia kama angeicheza nafasi hiyo kwa ufasaha.
Farid Mussa anaicheza nafasi hiyo kwa sasa. Ananikumbusha marehemu Said Mwamba ‘Kizota’. Marehemu alikuwa na uwezo wa kucheza nafasi tatu kwa ufasaha. Alikuwa anaweza kucheza kama kiungo, beki wa kati au mshambuliaji.
Marehemu Method Mogella pia naye alikuwa ana uwezo wa kucheza nafasi mbalimbali kwa ufasaha. Alikuwa ana uwezo wa kucheza kama kiungo kwa ufasaha na pia kucheza kama mlinzi wa kati kwa ufasaha. Ni kama ilivyo kwa Hussein Amani Marsha. Mwingine alikuwa Mwanamtwa Kihwelo ‘Dally Kimoko’.
Elewa maana ya neno ufasaha. Sio kwamba alikuwa anacheza kwa sababu waliotakiwa kucheza hawapo, hapana, alikuwa anacheza kwa ufasaha mwingi pia. Kizota alikuwa na miguu yenye kipaji maridadi kutoka Mkoa wa Tabora, kama ilivyo kwa Mtwa anayetokea ukoo wa wanasoka kutoka Mkoa wa Iringa.
Majuzi nilikuwa nalalamika kuona wachezaji wetu wa sasa wanashindwa kucheza nafasi tofauti kwa ufasaha kama Yannick Bangala anavyofanya. Labda Erasto Nyoni ameweza kufanya hivyo kwa nyakati mbalimbali ingawa sio kwa ufasaha sana kadhalika Shomari Kapombe, anayemudu kiungo, beki na ushambuliaji.
Na sasa Farid anaonyesha hilo. Anaweza kumuachia kocha wake, Nabi maumivu ya kichwa kama akiamua kuipenda nafasi hiyo. Sijui anafikiria nini, lakini kiukweli ni kwamba Farid anaweza kuwa mpinzani wa Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ katika nafasi hiyo hapa nchini kama akiamua kuipenda nafasi hiyo.
Kwanza anauona uwanja wa mapana zaidi tofauti na anavyocheza akiwa kama winga asilia. Anapocheza kama winga anajikuta yupo karibu na mabeki na karibu na ukuta wa wapinzani na nafasi yake kukimbia katika nafasi inakuwa ndogo.
Anapocheza katika nafasi yake ya sasa, Farid anauona uwanja katika mapana zaidi. Anapata nafasi ya kukimbia kwa hatua kumi bila ya kukabwa. Hata anapokabwa anajikuta tayari ana uamuzi kwa sababu anapata muda mwingi wa kufikiria akiwa njiani.
Kama Farid akiipenda nafasi yake basi anaweza kujizoesha kukaba. Anaweza kuwa bora zaidi katika eneo hilo kwani ana mapafu. Ana nguvu. Ni suala tu la kupenda kukaba. Kuna watu ambao hawafurahii kukaba na kuna watu ambao wanafurahia kukaba.
Kama akifurahia kukaba basi Farid atajikuta akiwa beki bora wa kushoto nchini, kwa sababu atakuwa na sifa zote. Atakuwa na sifa za kupanda pia atakuwa na sifa za kukaba. Naambiwa kwamba hata Nickson Kibabage wa KMC na timu ya taifa ya Tanzania alianzia kucheza kama winga kwa muda mrefu.
Kama kocha wake yeyote ataamua kuchezesha mabeki watatu wa kati pale nyuma basi Farid atanufaika zaidi kwa sababu 3-5-2 ni mfumo ambao unawawezesha mabeki wa pembeni kupanda na kushambulia kwa muda wote huku wale wale wa kati wakiwa tayari kuziba nafasi endapo kutatokea dharura yoyote.
Na sasa Farid ataanza kuiumiza kichwa Yanga. Mkataba wake unakaribia kukata roho mwishoni mwa msimu huu. Inawezekana katika nafasi yake halisi Farid atakuwa ameiridhisha Yanga kwa asilimia 70 tu. Kuna wakati wengi wanaamini kwamba Farid hakufikia matarajio.
Hata hivyo, kuna nyakati ambazo alionekana kuwa bora uwanjani. Lakini sasa Yanga wataumia kichwa kwa kuamini kwamba kama wataamua kuachana na Farid mwishoni mwa msimu basi watakuwa wameachana pia na beki mahiri wa upande wa kushoto.
Lakini Farid huyu huyu tukumbuke kwamba mara kadhaa ameweza kucheza kama kiungo asilia katika eneo la kiungo. Ilikuwa nyakati zile ambapo Saido Ntibanzokiza hakuwepo fomu kama ilivyokuwa sasa. Farid alikuwa anakipa kasi kiungo cha Yanga.
Kesi ya Farid inaweza kuwa ngumu zaidi kama kocha wa timu ya taifa, Kim Poulsen akiamua kumuita Farid katika kikosi chake kama beki wa kushoto na sio winga tena. Itakuwa vipi Yassin anarudi uwanjani na kucheza kama beki wa kushoto, lakini katika kikosi cha timu ya taifa Farid anaitwa kama beki wa kushoto?
Inachekesha kufikirisha kama Yanga wataamua kuachana na Farid mwishoni mwa msimu, halafu Simba wanaachana na Gadiel Michael na kumchukua Farid kama beki wa kushoto kwa ajili ya kusaidiana na Tshabalala katika nafasi hiyo. Simba itakuwa na mabeki bora wawili wa kushoto.
Somo la Farid ni wachezaji kuweza kuzipenda nafasi mbalimbali uwanjani. Lakini ni jukumu la makocha pia kuwajaribu wachezaji katika nafasi mbalimbali uwanjani. Wakati fulani niliwahi kuwalaumu baadhi ya wachezaji wetu kustaafia katika nafasi moja.
Kwa mfano, Shadrack Nsajigwa kwa muda mrefu wa maisha yake alikuwa anacheza kama beki wa kulia. Umri ulipomkamata angeweza kwenda kupumzika katika eneo la kiungo lakini alijikuta akiendelea kufukuzana na mawinga hatari hata wakati umri ukiwa umekwenda.
Kama angerudi kucheza kama kiungo angepumzika zaidi kwa sababu angecheza katika eneo ambalo asingekimbia sana kama alivyokuwa winga. Bahati nzuri kwake ni kwamba aliwahi kucheza nafasi hiyo akiwa shuleni, pia ana akili nzuri tu ya kucheza eneo hilo.
Sir Alex Ferguson aliwahi pia kumpumzisha Ryan Giggs katika eneo la kiungo baada ya kumtumikisha kwa muda mrefu kama winga. Alipoona kasi inaanza kupungua katika miguu ya Giggs akamuhamishia katikati acheze kama kiungo mshambuliaji.
Giggs akatumia siku za mwisho za maisha yake ya soka kuutuma mpira katika maeneo mbalimbali uwanjani kuliko kukimbia nao. Kama angeendelea kubakia kule kule katika winga angestaafu mapema zaidi kwa sababu kasi ilishamtupa.