Baadhi ya wanaharakati wameandamana katika Jiji la London nchini Uingereza na kuliteka jumba la kifahari linalomilikiwa na Bilionea wa Urusi, Oleg Deripaska aliyewekewa vikwazo hivi karibuni na Serikali ya Uingereza.
Wanaharakati hao wamekosoa muda wa kipindi cha miezi 6 unaoweza kuchukua kutekeleza vikwazo vya Uingereza dhidi ya washirika wa karibu wa Rais wa Urusi, Vladimir Putin ambaye naye pia amewekewa vikwazo kadhaa vya kiuchumi kutokana na kuanzisha vita nchini Ukraine.
Bilionea huyo anashutumiwa kuwa mshirika wa Putin na kusaidia Kremlin katika shughuli za ushawishi wa kigeni ambapo wiki iliyopita alipigwa marufuku ya kufungiwa mali na kusafiri pamoja na mabilionea wengine sita wa Urusi, akiwemo mshirika wake wa zamani wa biashara Roman Abramovich.
Waandamanaji wanaopeperusha bendera ya Ukraine wamechukua jumba hilo la kifahari na kueleza kuwa wanataka kulitumia kuwahifadhi wakimbizi kutoka Ukraine wanaokimbia vita vinavyoendelea kati ya nchi hiyo na Urusi.
Wanaharakati hao waliweka bendera ya Ukraine na kubandika mabango katika nyumba hiyo yaliyoandikwa maneno yanayosomeka: “Mali hii imekombolewa”.
Polisi wa Uingereza wamewakamata wanaharakati wanne waliokuwa wameandamana huku mmoja kati yao akiliambia Shirika la Habari la AFP kwa njia ya simu kuwa “Sisi ni mstari wa ukombozi wa mali, ndivyo tunavyofanya katika ukombozi.”
Wakati huohuo, wanaume watatu nchini Ufaransa walihojiwa na polisi siku ya Jumatatu baada ya kuingia katika jumba moja linalomilikiwa na mkwe wa zamani wa Putin na kupeperusha bendera ya Ukraine katika Mji wa Biarritz uliopo Kusini mwa Ufaransa.
Huku video ya YouTube ikionesha mmoja wa wale waliokamatwa akipeperusha bendera ya Ukraine kutoka katika jumba hilo ambapo bendera hiyo iliandikwa maneno yaliyosomeka: “Nyumba ya watu iko tayari kuwapokea wakimbizi kutoka kwa serikali ya Putin”.
“Damu ya watu wa Ukraine iko mikononi mwao. Wanapaswa kunyongwa vichwa vyao kwa aibu, uungaji mkono wetu kwa Ukraine hautayumba. Hatutasimama katika misheni hii ya kuongeza shinikizo kwa serikali ya Putin na kuzima pesa kwa mashine yake ya kikatili ya vita ” alisema Truss.