Mwanza. Kwa miaka kadhaa sasa, ‘Mfalme Zumaridi’ ambaye jina lake halisi ni Diana Bundala, ni miongoni mwa wahubiri wa dini wanaovuma ndani na nje ya Jiji la Mwanza.
‘Mfalme Zumaridi’ (39) ambaye pia hujiita mungu wa duniani amesikika akitoa huduma ya maombezi, mahubiri na hata tiba kwa magonjwa kadhaa anayodai kuwa na uwezo wa kuyaponya.
Ingawa hakuna maelezo mengi kuhusu historia yake, Diana alizaliwa Oktoba 9, 1983 katika kijiji cha Maganzo Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga.
Imezoeleka kuona historia ya elimu ya dunia na dini ya viongozi wa madhehebu mbalimbali nchini, lakini kwa ‘mfalme Zumaridi’ suala la historia yake jinsi alivyoingia kwenye masuala ya kuhubiri dini hadi sasa ni giza nene, kwani licha ya kuendesha ibada zinazohudhuriwa na mamia ya waumini, haijulikani ni wapi aliposoma na kufuzu masomo ya dini.
Hata hivyo, kukosekana kwa historia yake hakujamzuia ‘mfalme Zumaridi’ kuvuna idadi kubwa ya waumini katika kanisa lake lililopo eneo la Iseni jijini Mwanza ambalo kwa sasa limesitisha huduma baada ya kufungwa na Serikali miaka mitatu iliyopita.
Kabla ya kufungwa, kanisa hilo lilikuwa likiendesha ibada za kawaida za kila siku zikifuatiwa na maombezi ya kutwa na usiku kucha kwa wenye matatizo na mahitaji mbalimbali.
Ibada inavyofanyika
“Japo mimi si muumini, naishi jirani na kanisa lake mtaa wa Iseni; kila siku tulishuhudia waumini wake wakilala chini kifudifudi na yeye kutembelea juu yao kwa kuwakanyaga mgongoni hadi afike madhabahuni,” alisema Rosemary Paulo, mkazi wa mtaa wa Iseni jijini Mwanza
Alisema wakati watu wengine wasiokuwa waumini wa kiongozi huyo wanashangazwa na aina hiyo ya mapokezi ya muhubiri huyo wakati wa kuanzia ibada, waumini wake waliona fahari kubwa pindi ‘mfalme Zumaridi’ anapopita kwa kuwakanyaga migongoni.
Alisema muda wote kabla ya kuingia kanisani, hulindwa na kundi la vijana, wake kwa waume waliovalia suruali au sketi nyeusi huku juu wakiwa wamevaa mashati au magauni meupe na tai nyeusi.
“Wao wanawaita vijana hao ni askari wa Makerubi na Maserafi,” alisema Halima Jumanne, jirani mwingine anayeishi eneo la Iseni.
Zawadi, kuchinja ng’ombe
Mmoja wa waumini aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina alisema wanamuamini kuwa ni ‘mfalme’, mungu wa duniani na mfariji wao mkuu katika maisha na shughuli zote.
“Amekuwa msaada mkubwa kwetu siyo tu katika masuala ya imani, bali hata mahitaji ya kila siku ya familia zetu ikiwemo msaada wa chakula, mavazi na ada ya shule kwa watoto wetu. Mfalme anajitoa sana kwa ajili yetu. Huyu ndiye mfariji wetu mkuu,” alisema kwa hisia muumini huyo.
Alisema katika baadhi ya matukio, ‘mfalme Zumaridi’ huwafanyia sherehe kwa kuchinja ng’ombe wengi, kiasi cha waumini kushindwa kumaliza nyama ambayo hugawiwa hadi kwa majirani na wapita njia. “Kwetu sisi huyu ni mfalme, mungu na mfariji wetu mkuu; na pale nyumbani kwake ni ikulu,” alisema.
‘Mfalme’ akilia, nao hulia
Pamoja na kujipanga mistari miwili wakati wa kumpokea na kuagana na ‘mfalme’ wao, waumini hao hutakiwa kucheka, kutabasamu au kulia kila mkuu wao anapofanya hivyo.
“Kuna siku nilihudhuria ibada pale kanisani baada ya sifa za ‘mfalme Zumaridi’ kuenea kuwa ana uwezo wa kuponya maradhi mbalimbali; nilikuwa na mtoto mgonjwa aliyeugua muda mrefu, nikaamua kumpeleka pale. Lakini nilikosea taratibu za ibada hadi wazee wa kanisa wakaniijia kunihoji iwapo mimi ni mgeni,” alisema Yohana Emanuel, mkazi wa mtaa wa California, Nyegezi jijini Mwanza.
Alisema baadaye alipelekwa pembeni na kuelekezwa kufuata matendo na matukio yote ya kiongozi kwa kucheka, kutabasamu au kulia pale alipofanya hivyo.
“Tangu siku ile sikurudi tena kutokana na niliyoyashuhudia ikiwemo lile la waumini kulala chini na kiongozi kupita juu yao kwa kuwakanyaga migongoni,” alisema Yohana.
Serikali kusitisha ibada
Novemba 18, 2019 Serikali kupitia aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana wakati huo, Dk Philis Nyimbi alisitisha ibada na kufunga shughuli zote zilizokuwa zikifanyika katika kanisa la ‘mfalme Zumaridi’ baada ya kubainika kasoro kadhaa ikiwemo ukiukwaji wa mila, desturi, tamaduni na mafundisho ya kiimani.
Katika amri yake wakati huo, Dk Nyimbi alisema Serikali ilibaini kuwa shughuli za kanisa hilo zilikuwa zinakiuka sura ya 337 ya sheria na kanuni za usajili na uendeshaji wa vyama na jumuiya za kijamii.
Kanisa hilo pia lilibainika kutumia Katiba ya Kanisa la Pentecoste ambalo usajili wake unaonyesha kuwa liko jijini Dar es Salaam.
Eeneo lingine lililoleta ukakasi hadi Serikali kufikia uamuzi wa kusitisha ibada na kulifunga ni kitendo cha kiongozi huyo kujiita mungu wa duniani huku akijitambulisha kama ‘mfalme’ wakati yeye ni wa jinsi ya kike kinyume cha mila, desturi na tamaduni zinawatambua watawala wa kimila wa kike kama malkia.
Ibada kuhamia nyumbani
Baada ya Serikali kusitisha ibada na kufunga kanisa, ‘mfalme Zumaridi’ alihamishia shughuli zote nyumbani kwake mtaa wa Bugugu eneo la Mkolani jijini Mwanza.
Akizungumza na Mwananchi jana, Suzan Mwamjungu, mkazi wa mtaa wa Buguku yalipo makazi ya kiongozi huyo alisema shughuli za ibada na maombezi zinafanyika nyumbani kila siku mchana na usiku.
“Wanafanya ibada na maombezi kuanzia asubuhi hadi usiku wa manane; kila siku tulikuwa tunawaona watu wakiingia na kutoka humo ndani kwa ajili ya ibada na maombezi yanayoambatana na kupiga filimbi, matarumbeta na mavuvuzela,” alisema Suzan
Kutiwa mbaroni
Baada ya video iliyoonyesha askari polisi walioingia nyumbani kwa ‘mfalme Zumaridi’ wakisongwasongwa na ‘askari wa makerubi na maserafi’ wanaomlinda kiongozi wao, Jeshi la Polisi lilitangaza kumtia mbaroni kiongozi huyo ‘kwa mahojiano kuhusu tuhuma kadhaa ikiwemo usafirishaji haramu wa binadamu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ramadhani Ng’anzi alisema Diana anayeshikiliwa na waumini wake 149 waliokutwa nyumbani kwake pia anatuhumiwa kuendesha shughuli za ibada na maombezi kinyume cha sheria.
Tuhuma nyingine inayomkabili ni kuwafungia waumini wake nyumbani kwake na kuwatumikisha kinyume cha sheria.
Katika orodha ya waumini waliokutwa wakiwa wamefungiwa nyumbani kwa kiongozi huyo wa dini ni wanawake 92 na wanaume 57 miongoni mwao wakiwemo watoto 24 wenye umri kati ya miaka minne hadi 17.
“Tunaendelea na uchunguzi kuhusu tuhuma zinazomkabili; tufamfikisha mahakamni pindi upelelezi utakapokamilika,” alisema Kamanda Ng’anzi
Makerubi na Maserafi
Akizungumzia walinzi wa ‘mfalme Zumaridi’ wanaojiita askari wa Makerubi na Maserafi, Askofu Dk Sekelwa alisema kiimani, hao ni viumbe aina ya malaika wanaozunguka kiti cha enzi cha Mungu ambao kazi na jukumu lao ni kumuabudu na kumsifu Mungu.
“Kiimani, Makerubi na Maserafi wako mbinguni na si kuja duniani na mafundisho au madai kwamba wanawashukia wanadamu ni jambo lisilokuwepo katika mafundisho yote ya kidini,” alisema Askofu Sekelwa.