KAMATI ya Kudumu ya Bunge Yabaini 'Madudu Kibao' Mradi SGR




KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imebaini matatizo katika ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kipande cha tano kati ya Fela mkoani Mwanza na Isaka mkoani Shinyanga.

Miongoni mwa matatizo yaliyobainika ni kasi ndogo ya ujenzi, kutoonekana mitambo ya ujenzi eneo la mradi, kutolipwa fidia ya mashamba ya wananchi pamoja na vijana wazalendo kubaguliwa katika ajira za mradi huo.

Wajumbe wa kamati hyo walibainisha dosari hizo jana katika ziara waliyofanya ya kutembelea mradi huo kati ya Mwanza na Isaka.

Mjumbe wa kamati hiyo na Mbunge wa Kyela, Ally Msagila, akizungumza katika kikao cha majumuisho ya ziara hiyo, alisema mtu akiangalia kwa macho anaona kazi hairidhishi.

Alisema mradi huo ambao utagharimu Sh. trilioni 3.6 unahitaji kusimamiwa kwa karibu ili ulete tija.


Mbunge wa Sumbawanga, Aeshi Hilary, alisema wabunge hawajaona vifaa vinavyotumika katika ujenzi eneo la mradi na kwamba hali hiyo inaleta wasiwasi.

Mbunge wa Viti Maalumu, Sophia Mwakagenda, akizungumza katika ziara hiyo, alisema mradi huo unasuasua na hadi sasa umefika asilimia nne tu tangu ulipoanza Mei mwaka jana.

Alisema malalamiko ya wananchi katika mradi huo yamekuwa mengi ikiwamo kukosa ajira pamoja na kutolipwa fidia ya mashamba yao eneo la Fela ili kupisha mradi huo Sh. milioni 800.


Akijibu hoja za wabunge hao, Meneja wa Mradi huo kutoka Shirika la Reli (TRC), Machibya Masanja, alikiri ujenzi huo kufikia asilimia 4.46 huku tuta linalobeba reli likiwa limefikia asilimia 10.

Meneja huyo alisema malipo waliyotoa kwa mkandarasi ni asililimia 15, sawa na Sh. bilioni 376.4.

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Atupele Mwakibete, akijibu baadhi ya hoja za wabunge, alisema serikali imetenga Sh. trilioni 14.5 kukamilisha ujenzi wa SGR kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza.

Alibainisha kuwa mpaka sasa serikali imetumia Sh. trilioni 7.7 na hakuna mkandarasi anayedai huku akiahidi serikali itaangalia njia nzuri ya kuwapatia ajira vijana wazalendo ili wanufaike na mradi huo.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Seleman Kakoso, aliitaka TRC kusimamia mradi huo kwa uzalendo ili wananchi wanufaike nao.

Alisema mradi huo umetoa kiasi kidogo cha huduma za jamii ambacho ni Sh. bilioni 1.8 wakati fedha za kujenga mradi huo zinafikia Sh. trilioni 3.6.

Jana asubuhi kundi kubwa la wananchi katika eneo la Fela unakojengwa mradi huo, lilisimamisha msafara wa kamati hiyo, wakipaza kilio chao kuhusu kunyimwa ajira katika mradi huo na wengine kutolipwa fidia ya maeneo yao.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad